Mbunge Ataka Mashine ya Kuwapima Wanaume Wasiofanyiwa Tohara
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Jackline Ngonyani ametaka wabunge ambao hawajafanyiwa tohara kuchunguzwa na wakibainika wafanyiwe, akibainisha kuwa hiyo ni mbinu mojawapo kupambana na maambukizi ya Ukimwi.
Jackline ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 7, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa taarifa ya kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi.
Amesema kwa utafiti ambao umefanyika unaonyesha wanaume ambao hawajatahiriwa wamekuwa wakiambukiza magonjwa mbalimbali, ukiwemo Ukimwi kwa asilimia 60.
Mbunge huyo alikatishwa na mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aliyempa taarifa kwamba hata Bunge la Kenya liliweka wataalam mbele ya mlango wa Bunge, wale waliobainika hawajatahiriwa walipata tiba.
“Ni sahihi kabisa Spika unaweza kuchukua utaratibu huo ili kuepuka maambukizi ya Ukimwi,” amesema Selasini.
Baada ya taarifa hiyo, Jackline aliendelea kuzungumza akibainisha kuwa zoezi hilo ni vyema lianzie kwa wabunge na watakaobainika hawajatahiriwa wafanyiwe tohara mara moja.
Amesema pia wasiofanyiwa tohara wamekuwa wakiambukiza kansa ya kizazi kwa wanawake.
Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia alimpa taarifa Jackline kuwa wakati akitoa hoja ya wabunge wanaume wapimwe mikono sweta, hawakuwepo ndani ya ukumbi wa Bunge ili waweze kuunga mkono hoja hiyo.
Ghasia amesema jambo la kusikitisha wasiofanyiwa tohara wanakwenda kuambukiza magonjwa wanawake.
Hata hivyo, mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku ‘Musukuma’ alitoa taarifa akisema si jambo jema kutaka wabunge wasiofanyiwa tohara waweze kutambulika na kufanyiwa.
“Lakini pia takwimu zinaonesha kuwa hata wanawake waliokeketwa pia wanachangia maambikizi ya Ukimwi. Hivyo tuwekewe mashine ili wakati tunapima wanaume wasiotahiriwa basi tupime na wanawake waliokeketwa,” amesema.
Post a Comment