0

Ngome ya vijana ya Chama cha ACT-Wazalendo imelitaka Jeshi la Polisi kuanza kuchukua hatua kwa mambo yanayofanywa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kabla hawajaanza kuwashughulikia.

Wameyasema hayo leo Jumapili Februari 10, 2019 ikiwa ni siku chache tangu kusambaa kwa kipande cha video kilichokuwa kikionyesha vijana hao wakishangilia na kutamka maneno kuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu apigwe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mratibu wa ulinzi na usalama ngome ya vijana Taifa, Kudra Garula amesema vijana hao wamekuwa wakitoa maneno ya kichochezi na kuashiria vitendo vya uvunjifu wa amani katika mikutano yao lakini hakuna hatua zozote za kisheria zinazochukuliwa.

"Kukaa kwetu kimya kwa muda mrefu ilikuwa ni kuwapa nafasi polisi kufanya kazi yao ambayo kikatiba ni jukumu lao kuhakikisha amani, ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Ukimya wao unatia mashaka na kuonyesha upendeleo unaoweza kupelekea machafuko katika nchi yetu," amesema Garula.

"Sasa wasitake tufike huko, tumekuwa tukijitahidi kujibu mapigo kwa njia ya amani kwa kufuafa taratibu zote zinazostahili pale tunapoona kukosewa lakini hatuoni matunda sasa tutaanza kujibu mapigo kwa njia tofauti,"

Amesema jeshi hilo hata linapopewa taarifa juu ya kitu fulani limekuwa halifuatilii na kutolea majibu kwa wakati kitendo kinachoashiria kuwa ni maagizo.

"Hii si mara moja, tumeshuhudia kwa mbunge Tundu Lissu na Ben Saanane kabla ya kuwakuta matatizo walikuwa wakisema wanafuatiliwa na kutishiwa uhai lakini hakuna mtu aliyetolea majibu suala hilo," amesema Garula.

Amesema kabla yakufanya hivyo wataandika barua maalum na kuipeleka kwa Waziri Mkuu na nakala kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, IGP, DCI, taasisi za dini, asasi na taasisi za ndani na nje ya nchi na balozi mbalimbali kuwaeleza juu ya viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na UVCCM.

Post a Comment

 
Top