0
Mawasiliano Ya Barabara Ya Dodoma- morogoro Yarejea Baada ya Daraja la Dumira Kuathiriwa na Mvua
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa, amewahakikishia wananchi na watumiaji wa  barabara ya Morogoro-Dodoma kuwa mawasiliano  ya barabara hiyo sehemu ya maingilio ya daraja la Dumila yamerudi kama ilivyokuwa awali.

Kauli hiyo ameitoa jana mkoani Morogoro, alipofika darajani hapo kujionea athari za mvua zilizosababisha kubomoka kwa daraja hilo na wananchi kushindwa kutumia barabara hiyo kwa  takriban masaa saba.

“Kama mlivyoshuhudia tangu asubuhi tumeanza kazi za kurudisha mawasiliano katika barabara hii, matengenezo yamekamilika na wananchi tayari wameshaanza kutumia barabara”, alisema Naibu Waziri Kwandikwa.

Aidha, ameupaongeza Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kampuni ya ujenzi ya Yapi Merkez na wadau wote waliojitokeza katika kuhakikisha wanashirikiana bega kwa bega ili kurudisha mawasiliano katika eneo hilo.

Aliongeza kuwa katika kuhakikisha mawasiliano ya barabara yanakuwa imara,  Serikali ipo katika mpango wa kuboresha barabara hiyo ambapo kwa sasa wataalam wanafanya usanifu wa barabara hiyo na pindi usanifu huo utakapokamilika basi ujenzi wake utaanza mara moja na wataanza na sehemu korofi.

Awali akitoa taarifa kwa Naibu Waziri huyo, Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Steven Kebwe, alisema kuwa uongozi wa mkoa ulifika eneo la tukio na kuanza kushirikiana na TANROADS mkoa kuhakikisha miundombinu hiyo inarejea mapema.

Aliwataka wananchi kujitolea kupanda matete na magugu maji katika eneo hilo  ili kuelekeza maji yanayopita katika mto huo kuelekea sehemu husika.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro, Mhandisi Dorothy Ntenga, alisema kuwa kazi zilizokuwa zikifanyika katika maingilio ya daraja hilo ilikuwa  ni kuweka mawe makubwa na kokoto sehemu iliyobomoka.

Alifafanua kuwa kutokana na sehemu hiyo kuwa na maji mengi na mchanga mwingi, wamefikiria kufanya usanifu wa daraja hilo utakaoleta suluhisho la kudumu.

Post a Comment

 
Top