0
Hofu imetanda kufuatia kusambaa kwa taarifa kuwa kuna biashara ya viungo vya maiti inayofanyika kwenye maeneo ya makaburini, Uwazi linaripoti.

Makaburi yanayotajwa kwenye biashara hiyo ni Kinondoni na Sinza jijini Dar.

 Taarifa hizo zilidai kuwa, biashara hiyo inadaiwa kufanywa na baadhi ya wafanyabiashara kwa kushirikiana na vijana wanaotoa huduma za kuchimba makaburi katika maeneo tajwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika vilivyozungumza na Uwazi, taarifa hizo zilidai kuwa, viungo hivyo vinauzwa kwa bei chee kabisa.


Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.

“Kutokana na hali ya kimaisha kuwa ngumu, kuna vijana, wale wanaotoa huduma ya kuchimba makaburi ‘gravediggers’ au kuyafanyia usafi, inasemekana pia wanauza viungo vya maiti. Nasikia ishu hiyo ipo hasahasa kwenye Makaburi ya Kinondoni na Sinza-Makaburini,” alidai mmoja wa watoa taarifa wetu, Fresha Mariki, Mkazi wa Sinza- Palestina, Dar.

 “Mimi nadhani ni kwa ajili ya kuvitumia viungo hivyo kwenye biashara maana sasa hivi hali ni mbaya na kila mtu anafanya juu-chini kuhakikisha anapata chochote kwenye biashara.

“Kwa vyovyote jambo hili lina uhusiano mkubwa na mambo ya kishirikina,” alisema mtoa habari mwingine, Vincent Kabesi, mkazi wa Kinondoni-Kwamanyanya, Dar.

 Baada ya kuelezwa juu ya jambo hilo la kutisha, Uwazi halikuzipuuzia badala yake liliamua kuzifungia kazi kwa kwenda kwenye makaburi yaliyotajwa ili kufanya uchunguzi.

KINONDONI-MAKABURINI

Katika Makaburi ya Kinondoni, waandishi wetu walikutana na vijana wengi ambao wanajishughulisha na masuala ya kusaidia mazishi makaburini hapo.

Vijana hao waliwakaribisha waandishi wetu kwa bashasha kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kuchimba kaburi, kujengea, kusafisha makaburi na kutengeneza majeneza.



Wakiwa eneo hilo, waandishi wetu walijifanya wanataka huduma, hivyo walimuita mmoja wa vijana hao pembeni na kuzungumza naye.

Waandishi wetu walimweleza jamaa hiyo kuwa wanahitaji kiungo cha binadamu kwa bei yoyote ile kwa sababu walikuwa wamepewa dili.

 Awali, kijana huyo alionekana kushtuka, lakini baada ya kumuondoa wasiwasi, aliwaambia kwamba wanaweza kupata kiungo chochote cha maiti kwa sharti la kulifanya jambo hilo kwa siri kubwa na endapo watatoa kiasi cha shilingi laki mbili.

 Wakati wa majadiliano hayo, Uwazi lilikuwa likirekodi mazungumzo kati yake na kijana huyo ambaye alikuwa akijinasibu kwa vitu vingi huku akiongeza kwamba watu wengi, tena wazito, hufika makaburini hapo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ishu hiyo ya kuhitaji viungo vya maiti, kutupa vitu vyao vya kiganga makaburini au kuvunja nazi maeneo hayo.

 Bila kusema kama huwa wanawauzia viungo hivyo, jamaa huyo alijikuta akitoboa siri kuwa viungo vinavyouliziwa zaidi na watu hao ambao wengi ni wafanyabishara wakubwa na wanasiasa ni vidole vyote, viungo vya sehemu za siri, fuvu la kichwa na vinginevyo kama vile kipande cha sanda.

 SINZA-MAKABURINI

Baada ya uchunguzi wa kina kwenye makaburi hayo ya Kinondoni, waandishi wetu waliweka kambi kwenye Makaburi ya Sinza-Makaburini ambako nako walifanikiwa kuzungumza na vijana waliowakuta makaburini hapo ambao pia hali ilikuwa vilevile.

Kwa upande wa makaburi hayo, waandishi wetu walizungumza na vijana wawili ambao walisema kuwa, wenyewe wanaweza kufanya biashara hiyo kwa kiasi cha shilingi hata laki moja na kwamba wana mfuko ambao una viungo vingi waliouchimbia chini. Zaidi waliongeza kwamba, wao hufanya hivyo kwa waganga na watu wanaopenda masuala ya kishirikina.

POLISI WANAUJUA UHALIFU HUU?

Uchunguzi ulipokamilika, Uwazi lilimtafuta Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, DCI Robert Boaz lakini simu yake iliita bila kupokelewa. Likamgeukia Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Jumanne Muliro na kumuelezea kinagaubaga juu ya uchunguzi huo.

 Katika mazungumzo yake na Uwazi, Kamanda Muliro alisema kuwa, hana taarifa hizo na kwamba kwa kuwa alizipata kutoka kwa mwandishi wetu, basi atazifanyia kazi.

“Kiukweli sijasikia kabisa kuhusu suala hilo, kwa kuwa mmeniambia nitazifanyia kazi,” alisema Kamanda Muliro.

MEYA WA UBONGO

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alipoulizwa alisema: “Sina taarifa ya suala hilo, kikubwa mimi nitazifanyia kazi taarifa hizi ambazo mnanipa.”

NENO LA UWAZI

Gazeti hili linalaana vikali vitendo hivi kwa sababu ni kinyume na maadili, haki za binadamu na sheria za nchi. Pia linaviomba vyombo vya dola kufuatilia na kuwatia nguvuni wote wanaoshiriki vitendo hivi hasa pale itakapobainika kwamba taarifa hizo zina ukweli ndani yake.

STORI: WAANDISHI WETU | GAZETI LA UWAZI

Post a Comment

 
Top