0
Waziri Mkuu: Sekta Ya Kilimo Kuleta Mageuzi Ya Kiuchumi
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema sekta ya kilimo ina nafasi kubwa ya kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini iwapo changamoto zinazoikabili kama za upatikanaji wa pembejeo, mbinu na miundombinu duni ya uzalishaji, usafirishaji, uchakataji wa mazao na masokozitafanyiwa kazi kwa wakati.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Machi 19, 2019) wakati akifungua ofisi ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa Kanda ya Ziwa. Ameutaka uongozi wa benki hiyo ushirikiane na wadau wengine kutatua changamoto za kilimo nchini ili ndoto ya kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 itimie.

Waziri Mkuu amesema bado sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zimeendelea kukabiliwa na changamoto nyingi ambazo kwa kiasi kikubwa zimesababisha ufinyu wa tija hususan kwa wakulima wadogo, hivyo amewaagiza viongozi wa TADB waendelee na kasi ya utoaji huduma ili kuwafikia wakulima na wafuaji wengi zaidi nchini.

“Endeleeni kufanya kazi na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuweka na kutekeleza mipango ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima, wafugaji na wavuvi nchini. Pia panueni zaidi wigo wa huduma hususan utoaji wa mikopo katika kuendeleza miradi ya miundombinu ya kilimo, ufugaji na uvuvi na kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo kwa lengo la kuinua uzalishaji”.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kwa kuwa Benki Kuu ndiyomdhibiti mkuu wa mabenki nchini inao wajibu wa kutambua umuhimu wa kuandaa kanuni mbadala na sera za fedha ambazo ni rafiki kwa benki za mandeleo ya kilimo na ujasiriamali.

Amesema lengo ni kurahisisha utoaji wa huduma ya mikopo ya kibiashara tena yenye kuvutia kwenye sekta ya kilimo, hivyo ameitaka Benki Kuu iangalie namna ya kushirikiana na wadau hususan wa kilimo kuandaa kanuni maalumu za usimamizi angalifu wa fedha ambazo zitazingatia mazingira halisi ya kilimo na changamoto zake.

“Sambamba na kushughulikia sera au kanuni ambazo zinarahisisha kufanya biashara katika kilimo, Benki Kuu, pia inatakiwa kuendesha zoezi hilo bila kuhatarisha utulivu wa kifedha na kujihami na madhara na hatari zinazoambatana na ukopeshaji”.

Nae, Naibu Waziri wa Kilimo, ….Bashingwa amesema ufunguzi wa benki hiyo kwa Kanda ya Ziwa ni hatua nzuri ambayo inakwenda kuwasogezea huduma wakulima, hivyo ameutaka uongozi wa benki hiyo uandae utaratibu wakuwafundisha wakulima namna ya kuandika maandiko kwa ajili ya kuomba mikopo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine amesema hadi kufikia Februari 28, mwaka huu benki ya TADB imefanikiwa kukuza mtaji wake na kufikia kiasi cha sh. bilioni 68 ikiwa ni ongezeko la asilimia 13 kutoka mtaji wa sh. bilioni 60 uliotolewa na Serikali mwaka 2015.

Mkurugenzi huyo amesema ukuaji wa mtaji wa benki hiyo umechangiwa na malimbikizo ya faida iliyotengenezwa katika kila mwaka wa fedha tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2015, kutokana na utoaji wa mikopo ya kimkakati inayotolewa kwa wateja wao.

“Kilimo ‘kinabenkika’ kwani katika msimu wa pamba wa mwaka 2018 TADB ilitoa mkopo wa gharama nafuu ili kufanikisha ununuzi na usambazaji wa viuatilifu vya zao la pamba kwa wakulima katika mikoa 17 ikiwemo yote ya Kongani ya Kanda ya Ziwa na wilaya 49 nchini”.

Amesema mkopo huo ulichangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la uzalishaji, ambapo kwa msimu wa pamba wa mwaka 2018, mavuno ya pamba yaliongezeka na kufikia tani 221,600 ikiwa ni ongezeko la asilimia 67 ikilinganishwa na tani 133,000 zilizozalishwa msimu wa mwaka 2017.

Baada ya kufungua ofisi hiyo ya TADB kwa Kanda ya Ziwa, Waziri Mkuu alikabidhi matrekta 16 aina ya URSUS kwa vyama vya msingi, ambapo viongozi wa vyama hivyo wameishukuru Sekali kwa uamuzi wake wa kuwajali wakulima kwa kuwapatia huduma muhimu zikiwemo  pembejeo.

Post a Comment

 
Top