0
Shaidi wa Kesi ya Malinzi Ashindwa Kutokea Mahakamani
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, jana ilishindwa kuendelea na kesi inayowakabili waliokuwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kushindwa kuleta mashahidi huku wakili wake akishindwa kufika mahakamani hapo.



Jana Jumanne, kesi hiyo ilitarajiwa kuendelea kusikilizwa kwa upande wa kutoa ushahidi ambapo
awali tayari mashahidi 11 wametoa ushahidi wao.



Wakili wa Serikali, Imani Nitume ambaye alimuwakilisha Wakili Leonard Swai, aliiambia mahakama hiyo kuwa, Wakili Swai alishindwa kufika kutokana na kuwa na majukumu mengine.



Wakili huyo aliiambia mahakama kuwa kutokana na Swai kutokuwepo na ni wakili ambaye pia anaandaa mashahidi ndiyo maana wameshindwa kuja na shahidi ingawa shahidi ambaye alitakiwa kuja naye aliomba udhuru.



Aidha wakili ambaye aliwawakilisha washitakiwa, Kashindye Thabiti aliiambia mahakama kuwa upande wa serikali unapaswa kuhakikisha kuwa unaleta mashahidi hata watatu katika kesi ijayo.



Aliongeza kuwa kesi hiyo upande wa Takukuru wanatakiwa kutuma wawakilishi wao kwa sababu wapo wengi na hata kama Swai asipokuwepo yupo Kimaro ambaye amekuwepo tangu awali kesi hiyo ilipoanza au mawakili wao wengine.



Baada ya hayo yote kujiri, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Maira Kasonde, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 26 mwaka huu. Malinzi na wenzake, Celestine Mwesigwa ambaye alikuwa Katibu wa TFF na Mhasibu Nsiande Mwanga, wanakabiliwa na mashitaka 28, ikiwemo ya utakatishaji fedha Dola za Marekani, 173,335, na wako mahabusu kwa sababu mashtaka yao kisheria hayana dhamana

Post a Comment

 
Top