0
Mfanyabiashara aliyebambikiziwa kesi ya mauaji na Jeshi la Polisi, afunguka alivyokamatwa na kunyang’anywa mali zake
Mfanyabiashara, Mussa Sadiki aliyebambikiziwa kesi ya mauaji na Jeshi la Polisi mkoani Tabora, amefunguka alivyokamatwa na askari wa jeshi hilo, kunyang’anywa mali zake hadi kuingizwa mahabusu.


Mkuu wa Jeshi la Polisi
Akisimulia tukio hilo, mfanyabiashara huyo alidai kuwa Juni 11, mwaka jana, alifika Tabora majira ya saa saba mchana akitokea Dar es Salaam.
Sadiki anadai kuwa baada ya kufika mjini Tabora, alipanda gari kwenda Soko la Kachome mkoani humo kwa lengo la kukutana na mtu aliyekuwa akimdai Sh. milioni 1.6 .

“Nilikutana na mdeni wangu, lakini aliniambia nimsubiri kidogo anakwenda kutoa fedha kwa wakala, muda mfupi nikamwona askari polisi ambaye alinifuata na kuniuliza kama mimi ndiye Mussa Adamu Sadiki na baada ya kumjibu, nilikamatwa na kufungwa pingu,” Sadiki alieleza na kuongeza.

“Nilinyang’anywa mali zangu na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Tabora, nilipowauliza kesi gani inayonikabili, niliambiwa niendelee kukaa huko kituoni na nitajua wakati wakiendelea kuifuatilia”.

“Nikiwa kituoni hapo, alifika askari … (alitaja jina la askari polisi) majira ya saa 8:00 mchana ili kuhakiki mahabusu. Nilimuuliza huyo afande, ‘nina kesi gani iliyoniweka humu, ambayo hadi siku hiyo ilikuwa ni wiki ya pili?’ Aliniambia ninashtakiwa kwa kosa la kuvunja na kuiba ofisini.”


Sadiki alidai kuwa siku tano baada ya kupewa taarifa za kwamba anakabiliwa na tuhuma za kuvunja na kuiba, alichukuliwa na kupandishwa ghorofani huku akiwa amefungwa pingu mikono na miguu.

Alidai kuwa akiwa huko, alilazimishwa ashike kibao kilichoandikwa ‘unyang’anyi wa kutumia nguvu’ na akapigwa picha akiwa amekishika.
Alidai kabla ya kupigwa picha hiyo, alihoji kwanini wanamfanyia hivyo, huku wakiwa wamemfunga pingu, wakati watuhumiwa wengine hawakufanywa hivyo.

Niliambiwa nikishike kibao, nilitii wakanipiga picha na baadaye tulirudishwa kituoni, nilichukuliwa maelezo na baada ya muda nikafikishwa mahakamani, lakini nikaambiwa mashtaka yanayonikabili sitakiwi kujibu chochote,” Sadiki alidai.

“Nilisomewa mashtaka ambayo nilishtakiwa kwa kumuua, Thomas Jacob mnamo Juni 5, barabara ya kwenda Kazima, Ipuli mjini Tabora, niliambiwa nisijibu lolote. Juni 29, nikapelekwa gerezani.”

Sadiki alidai kuwa, awali akiwa kituo cha polisi, alikutana na mshtakiwa mwingine, Edward Nduli, ambaye baadaye aliachwa huru.

“Nilimkuta akiwa na kesi ya kuvunja na kuiba Kituo cha Polisi mjini (Kituo Kikuu cha Polisi Tabora). Nikiwa gerezani wiki mbili mbele, mahabusi mmoja alinitafuta na akanitolea jalada la kesi ambalo linaonyesha mimi ni mshtakiwa namba moja na mshtakiwa namba mbili ni Edward Nduli,” Sadiki alidai.

Alidai wakati kesi hiyo inaendelea mahakamani, alikuwa akifuatilia mali zake alizopokwa na askari polisi ambazo ni Sh. 788,000, simu tatu na nguo alizonunua Kariakoo jijini Dar es Salaam na kwamba alikuwa na nyaraka za kuthibitisha ununuzi wa vitu hivyo.


“Hizi mali nilinyang’anywa na askari ambao ni …. (alitaja majina ya askari polisi watatu),” Mfanyabiashara huyo alidai anakumbuka akiwa mahakamani, hakimu alimwambia hawezi kuandika madai ya vitu vyake kwenye faili la kesi ya mauaji na kumtaka atumie mbinu nyingine.

“Hakimu alinieleza niandike barua kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa na Mpelelezi wa Wilaya. Pamoja na kufanya hivyo, sikupata majibu hadi nimeachiwa kwa agizo la Rais John Magufuli, namshukuru sana kwa utendaji wake wa kazi.”

“Wamefuatilia suala langu, wamenibambika kesi ambayo sijaifanya, sasa hivi najisikia nina amani, nipo huru nimeachiwa na sina kesi ya mauaji niliyopewa kwa lengo la kuninyang’anya fedha zangu, namshukuru Rais Magufuli.”


“Waliniambia ninashtakiwa kwa kosa la kuvunja ofisi na kuiba, lakini hata jina la ofisi hiyo sikutajiwa. Baadaye nikapigwa picha, nikaambiwa nina kosa la unyang’anyi. Niliandika barua kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri Mkuu, Waziri wa Katiba na Sheria na kwa Rais Magufuli ambayo haikumfikia, lakini lilifika gazeti na Mwendesha Mashtaka (DPP) alikuja gerezani na kunionyesha gazeti,” Sadiki alidai.


Mfanyabiashara huyo alidai aliandika barua alipozipeleka ofisi ya Magereza, aliambiwa hawana mamlaka ya kuzichukua na kuzipeleka kwa waziri.

“Walinishauri nifuatilie kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) au Kamanda wa Polisi Mkoa. Nilizuiliwa na RCO nisiongee na waandishi wa habari mpaka atakaponikabidhi fedha nilizokuwa nadai. Nimekabidhiwa fedha, lakini vitu vingine nilivyokuwa navidai sijapewa,” Sadiki alidai.

Alitaja vitu anavyodai kutoka kwa Jeshi la Polisi kuwa ni suruali za vitambaa na jeans saba, simu tatu, redio za biashara ambavyo kwa pamoja alidai vina thamani ya Sh. milioni 1.66.

Mfanyabiashara huyo amefunguka hayo baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wiki iliyopita kufichua, jinsi baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi walivyombambika kesi ya mauaji mkazi huyo wa Tabora baada ya kumpoka mali zake.

Post a Comment

 
Top