Hizi ndio sababu 5 zinazowafanya wanaume kwa sasa kupenda tendo la ndoa kwanza na sio kuoa
Wanawake wengi kwa sasa wanalalamika namna wanaume walivyo kwenye mahusiano, wanasema wanaume wamepoteza moyo wa dhati wa kuwepo wenye mahusiano yaani “commitment”, wanaonekana kama hawana mapenzi tena, wao kila siku ni kuuliza tu tendo la ndoa, na kama halipati basi anaweza kuondoka muda wowote kuelekea huko anakolipata tendo hilo.
Hali hii inasumbua mahusiano mengi ya uchumba na wengine wamelazimika kuvunja uchumba, wakiwa karibia kuingia kwenye ndoa.
Wanawake hawa wanalalamika wakisema wako wapi wale wanaume wenye kiu ya ndoa? Wako wapi wale wanaume wenye kuongelea kutaka kuoa na kuanza familia na kuwapenda watoto wao? Wako wapi wale wanaume wenye kiu ya mafanikio na kudumisha maisha pamoja na wake zao, mbona kama wamemalizika na waliobaki wana kiu za kula bata tu “kufanya starehe” na kufanya mapenzi pasipo kumaanisha.
Yamkini na wewe unayesoma makala hii unajiuliza maswali haya pia. Wanawake wengine wamekuwa wakieleza kuwa wanaume waliobaki siku hizi ni wavivu, hawana hamasa ya maendeleo, atakuwa na wewe kama ana uhakika wa tendo la ndoa tu.
Leo nimekuja kuzungumza na wasichana na wanawake ambao nao wanamawazo na maswali kama haya, ni kweli vilio na malalamiko yenu ni ya kweli na tunasikitika pamoja kwenye hili lakini pia tafiti zinasema iko sababu ya hali hii.
Ni vyema mkafahamu kuwa kwa kiasi kikubwa mifumo au mbinu za mchezo wa mahusiano zimebadilika sana, nadharia za zamani nazo zinaonekana kubadilika na hii imewafanya wanaume wengi kubadili aina ya maisha yao.
Fuatilia sababu zifuatazo ili kulielewa hili sawia. Kumbuka kuwa sababu hizi zimetokana na majibu ya wanaume wengi kwenye tafiti;
Mgawanyo wa majukumu baina ya wanaume na wanawake umeingia doa.
Wanaume wa kawaida hupenda kufanya kazi ili kujitafutia kipato chao na familia, na wakitoka kazini au kwenye majukumu yao ya kila siku wanataka kupumzika na kufanya kile wanachojisikia kufanya iwe ni kulala, kuangalia televisheni, kusikiliza redio n.k na sio kukimbizana na vijishuhuli vya nyumbani kama vile kusaidia kupika, kusafisha vitu, kukaa na watoto na kazi nyingine ambazo wao wanaona sio zao.
Ndani yao wanakiu ya kuona wapenzi wao wanawakaribisha kwa upendo, kuwaandalia maji, kuwasaidia kuweka mazingira ya wao kupumzisha akili na mwili baada ya kula chakula, wanakiu ya kuona tabasamu, sauti nzuri, na ikiwezekana kupata penzi. Kwao hali hii kuwapa nguvu tayari kuwaandaa na siku nyingine ya kesho.
Tatizo linakuja pale mwanaume huyu anajikuta ameoa mwanamke mfanyakazi au mwenye majukumu mengi yamkini kumzidi hata mume, akikaa, akilala anawaza kazi, anawaza biashara anawaza miradi na vingine vingi, akirudi nyumbani mwanamke huyu anakuja amechoka na hajiwezi kimwili na kiakili kama vile vile alivyo mume wake, mke na mume wote wamechoka sana, mke na mume wote wana msongo wa mawazo na wanahitaji kupepewa maana hawajiwezi kwa kuchoka.
Mwanamke amechoka hana hamasa ya kufanya kazi ndogondogo za nyumbani au hata kuwashuhulikia watoto. Ulimwengu wa kazi na majukumu umeshamfanya mwanamke kuwa na misuli ya kukimbizana na maisha kama mwanaume.
Hali hii inawafanya wote wawili wanarudi nyumbani wamechoka kabisa na kila mmoja anauhitaji wa msaada wamwenzake wakati hakuna aliyetayari wala aliyena nguvu ya kumsaidia mwenzake. Katika hali kama hizi vijihasira na vihisia hasi huamka kwa urahisi sana na magonvi huweza kupenye hapohapo. Ule uwiano wa masaidiano umeshapotea na kilichoota ni hatari sana kwa mahusiano ya wawili hawa.
Wachunguzi wanasema ndio maana zipo jamii na imani fulani ambazo mke huachwa nyumbani akimsubiri mume wake na mume kazi yake ni kuhakikisha anafanya kila jitihada kuilisha na kuitunza familia, sio kwamba hawataki mke afanye majukumu ya baba la hasha, wanamuandaa kuweza kumhudumia mumewe vilivyo. Najua hoja za wengi pia zina mashiko kwamba wanawake wengine wangependa kukaa ka kuwasubiria waume zao ili wawaenzi lakini wanaume wengine wameshindwa kubeba majukumu yao kama wanaume na viongozi wa familia na hiyo imewalazimu wanawake kusimama na kufunga mkanda. Pamoja na hayo hali ya masumbufu haijapungua.
Wanaume hawapendelei kulipia kitu wanachoweza kukipata bure.
Ni dhahiri kabisa kwamba wanawake wengi sikuhizi hata wale wenye umri wa kuolewa wamejikita zaidi kwenye maisha ya starehe, wao ni kula, kunywa, kusafiri, kuvinjari usiku hadi kukuche wanakula maisha “wanakula bata”. Ngono imekuwa rahisi sana kwa wasichana wa umri mdogo na hata wanawake waumri wa kuolewa na pia wale walioko kwenye ndoa.
Unakuta mwanamke anakiu ya kuolewa na anasema wazi kuwa anatamani kuwa na mume lakini maisha nayoishi hayaendani kabisa na mke wa mtu, anashindwa kufahamu kuwa waoaji wengine ndio hao hao anashinda nao baa na kwenye majumba ya starehe, anashindwa kujua kuwa watu wanamwona na wanapata picha dhahiri ya namna na tabia aliyonayo. Vijana wanaona kama ngono inaurahisi wakuipata hivyo yanini akajitutumue kuanza michakato ya kulipa mahari? Kama unaweza kumwambia mwanamke aje kwako na akalala wiki pasipo shida, kunahaja gani ya kubeba kajukumu mengine ya zaidi? Waingereza wanasema “if you can affor a sousage why keeping a pig” (Kama unauhakika wa kupata nyama ya nguruwe kwanini uhangaike kumfuga?).
Usitegemee kuolewa na mtu mzuri, anayemaanisha na mwenye mapenzi wakati wewe haumaanishi chochote na penzi lako unagawa kwa yeyote huko nje. Kwa taarifa yako hata mwanaume aliyeko kihasarahasara anakiu ya kuwa na mke anayejiheshimu. Ningumu sana rafiki zako wa kiume wanakaa na wewe hadi kunakucha wanakurudisha kwenu au kwako halafu unadhani yuko kati yao atakaye kuja kusema anataka kukuoa, never!! Kila anayekuona anajua fika wewe sio mke ni mwanamke wa usiku, utakachokipata sanasana ni kufanya nao ngono, wakuache hapo waende zao kuoa wanawake wanaojielewa.
Majukumu ya baba kama kichwa cha nyumba yamebadilika
Kwa asili wanaume wameumbwa na kiu ya kutaka kuongoza, kutaka kuwa wasimamizi au wakurugenzi wakila kitu kwenye maisha yao, kwenye vipaji vyao, kwenye kazi zao, kwenye mahusiano yao na hata kwenye familia zao. Pamoja na kiu hii, kwa miaka ya karibuni hali imebadilika sana, maendeleo ya kijamii na kiteknolojia yamepunguza sana au kuondoa kabisa ule ukuu alokuwa nao baba kwenye familia yake.
Leo kwenye jamii nyingi hususani za magharibi baba hawezi tena kumuadabisha mtoto wake maana anaweza kumshtaki kwenye vyombo vya sharia au hata kumpeleka mahakamani. Leo katika jamii nyingi duniani, kwenye nchi zilizoendelea na hata hizi zetu zinazojikongoja, baba akisema atumie mamkala yake kama baba haiitwi tena mamlaka inaitwa unyanyasaji, na inaweza kumtokea mtu puani. Kila mke anataka usawa, ukifanya hivi mke atafanya vile, ukitaka hiki nayeye atataka kile, ndoa nyingi zimeshakuwa kama chama tawala na chama cha upinzani, wanandoa wengi wameanza kuishi kama taasisi sio kama wapenzi. Inasemekana kwamba kama ile kiu ya baba au mwanaume kuhangaika na kuwekeza jasho na akili yake kwenye familia yake ili aiongoze, awe kichwa imeoza au haileti faida basi hakuna anayeona umuhimu wa jitihada hizo tena. Imekuwa kama mfanya biashara anaona yanini kuwekeza ambako unauhakika patakupa hasara? Maana ya hii ni kwamba, hamasa ya wanaume wengi kuingia kwenye ndoa na hatimaye familia imeonekana kupungua na hivyo kulitafuta hitaji lao la asili ya tendo la ndoa nje ya ndoa.
Sheria za ndoa zinawabana wanaume zaidi
Wanaume wengi wameonyesha kuhofia sharia za ndoa kwa jinsi zinavyomgandamiza mwanaume na kumpa chapuo mwanamke. Wanaume wengi walioliongelea hili ni wa jamii ya nchi zilizoendelea na wachache ni wanchi zinazoendelea, wanasema wanahofu ya kuingia katika makubaliano tena ya maandishi ya kuishi pamoja maishani wakati makubaliano hayo yanamlemea mtu mmoja na sio wote, husuani pale mambo yanapoonekana kuharibika na tofauti zikaibuka baina ya wawili hawa.
Nyakati ndoa zinapovunjika na wanandoa wakalazimika kuchukulia mambo kisheria, mwanaume anahofia kupoteza kila anachoona ni chamuhimu kwake. Pamoja na kwamba upo ukweli kwamba hata kama mwanaume ndiye alitafuta lakini kuna watoto nao wanatakiwa kufaidika au kuendelezwa pamoja na kwamba ndoa imeshindikana, lakini wengine wanasema hatakama hatuna watoto, bado mwanamke ananafasi kubwa ya kumbana mwanaume kisheria. Pamoja na kwamba hofu hii haionekani sana kwa wanaume wanchi kama ya kwetu ila wapo baadhi wenye mtazamo huu. Kwa mtazamo huu sasa wengi wanaona bora waendelee kutafuta haja ya mwili “tendo la ndoa” halafu hayo mambo ya kuishi pamoja kama mume na mke yatajulikana huko mbele yasafari.
Hamasa ya kukua na kupevuka imepungua
Kuendesha familia au kuwa baba bora wa familia kunahitaji sana kumaanisha na kujitoa “commitment”, pasipo tabia hizi utabaki kuitwa baba au mume lakini lazima kutakuwa na mapungufu mengi sana na malalamiko kwenye familia kutoka kwa mke na hata watoto.
Kwa bahati mbaya inaonekana tabia hizi za kumaanisha zinapungua kwa kasi sana kwa wavulana wengi wenye umri mdogo na kuendelea hadi wanapokuja kuwa vijana wakubwa wanaotarajiwa kuingia kwenye ndoa zao. Vijana wanaonyesha uvivu na kukwepa majukumu wakiwa wadogo, wanachukia kazi na kuwa walegevu, wanapenda vitu virahisi na maisha ya anasa tu, mtu anatamani aangalie televisheni siku nzima na asifanye kazi. Familia nyingi zimepwaya kwenye suala la malezi, mvulana hapangiwi kazi wala majukumu ya kumfanya ajitume akiwa nyumbani.
Akitoka shule basi ni kucheza na kukaa tu na baadae wazazi hao hao waliomfundisha aina hiyo ma maisha wanakuja kuanza kulalamika eti huyu mtoto ameharibuka wakati wao wenyewe ndio waliomharibu. Kwabahati mbaya tabia hizi za kivivu na kilegevu na kukwepa majukumu huendelea hadi wanapoingia kwenye ndoa.
Mtu anaingia kwenye ndoa hata tabia ya kuhifadhi fedha yake kwa matumizi ya baadae auya dharura hana, akipata pesa ni starehe na safari za hapa na pale, mtu anapata mke hajui hata namna ya kumhudumia, mtoto akija ndio kabisa vita kila siku na mke wake maana nikama vile huyo mke wake analea watoto wawili wakati mmoja anajiita “baba”.
Inaumiza na kusumbua sana moyo. Kwa hali hii vijana wengi wanaogopa majukumu ya familia wanaishia kutaka tendo la ndoa tu, na hata kijana wa aina hii anapokuwa kwenye familia hafanyi kitu cha ziada, mke ndio jembe la nyumba, kijana yeye anasubiri kupewa unyumba tu. Kufuatia hali hii pia, baadhi ya wanawake wamekata tama au kuchukia kuolewa, wako tayari wafurahie maisha na kufanya mapenzi na mwanaume wanayemtaka ila pasipo masharti ya kudumu, akihitaji mtoto basi atampata kwa muda wake bila kujali baba ninani ama anaishi wapi. Hali imebadilika sana.
Hitimisho
Ulimwengu umebadilika sana na kuwa ulimwengu wa watu kupenda starehe, furaha na hamasa za muda mfupi pamoja na kiu kubwa ya kufanya mapenzi hovyo.Pamoja na kiu hiyo bado wengi wanahofia mahusiano ya kudumu na ndoa.
Wengi wanalia kwenye mahusiano au uchumba maana hakuna kumaanisha, ni kuumizana asubuhi, mchana, jioni nausiku. Kijana akiwa na msichana kwenye mahusiano na akawa na uhakika wa kupata tendo la ndoa basi anaweza hata kujisahau kuhusu kuoa, na vijana hawa kwakukwepa majukumu wanakimbilia kuishia kwa wasichana waliotapakaa kila sehemu ambao wao ni kula raha tu na wako tayari kumpa penzi yeyote aliye tayari kuwapa furaha, kinywaji, na starehe nyingine, wakati haya yanatokea, wale wanawake wachache wenye kumaanisha, wenye kujitunza, na wenye kiu ya kuwa na familia zao wanabaki wakisubiri nani mwanaume mwenye kumaanisha pia atakayekuja kutamani kuwa nao, maana kiukweli vijana wa aina hii ni wakutafuta, wamepungua sana.
Pamoja na kwamba baadhi ya sababu zilizotajwa hapo juu ni ngumu kuzizuia lakini zipo pia ambazo zinaweza kuzuilika kama ukiweza kufanya maamuzi yako vizuri na kwa ufasaha.
Mabadiliko ya tabia pia ni muhimu kwenye muktadha huu. Wasichana au wanawake mnaojitunza, msikate tamaa kabisa, pamoja na kwamba dunia imebadilika na wengi waovu ndio wanaoonekana wajanja, jipeni moyo, hakuna aliyejitunza akajuta, ila hao wengi mnaowaona huko wakijionyesha kama wenye furaha sana, ndani ya mioyo yao na katika nyakati wanazokuwa pekeyao, wanamajuto makubwa sana ndani yao.
Chanzo : http://chrismauki.co.tz
Post a Comment