Wabunge wa Upinzani Watishia Kupeleka Hoja ya Kutokuwa na Imani na Spika Job Ndugai
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imemtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutengua uamuzi wake wa kusitisha kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hata hivyo, imesema kama Spika hatatengua uamuzi wake watatumia kila njia za kibunge ikiwamo kuwasilisha hoja ya kumuondoa Spika kwa kutokuwa na imani naye.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa akiwa ameambatana na wabunge wa upinzani, msemaji wa kambi hiyo, John Mnyika, alisema kanuni za bunge zimeweka utaratibu wa kufanya maamuzi ndani ya Bunge na nje kupitia kamati mbalimbali.
“Kamati ya Bunge ya Uongozi haijawahi kukaa kikao chochote cha kusitisha kufanya kazi na CAG, huu uamuzi ni uamuzi binafsi wa Spika ambao kambi hatuungi mkono na hatukubaliani nao,”alisema.
Alitoa wito kwa Spika Ndugai kujitokeza kwa umma kueleza kuwa ni kikao gani alikaa na kina nani kufanya uamuzi huo.
Alisema kitendo cha Spika kutokukaa kikao na kamati zenye mamlaka kinasababisha maswali mengi.
“Uamuzi huo umeenda sambamba na kusambaratisha Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kamati hizo zimesitishwa kufanya kazi zake kuanzia 14-25 Januari, mwaka huu na kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, kamati zinamaliza kazi zake tarehe 25,”alisema.
Mnyika alisema Spika amesitisha kamati hizo kufanya kazi zao za kikatiba kwa mujibu wa ratiba ya Bunge.
“Tunapinga hatua hii na tunapinga huu uamuzi, tunataka Spika abadilishe mara moja huu uamuzi na kamati zikutane na kufanya kazi ya kikatiba,” alisema.
Aliongeza “Spika anasema kwa sababu CAG ameitwa tarehe 21 Januari kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa madai kuna mgogoro kati ya Bunge na CAG, wakati hakuna kamati ya bunge iliyotangaza Bunge lina mgogoro na CAG na kauli hiyo ni binafsi si kauli ya Bunge wala Taasisi ya Bunge.”
Alisema haiwezi kuwa kisingizio kwa kamati zishindwe kufanya kazi, haiwezekani spika akiwa na mgogoro na CAG kamati za bunge na Ofisi ya CAG zikasitishwa kufanya kazi.
Hata hivyo, alisema Januari 14, mwaka huu PAC kwa mujibu wa ratiba ilikuwa inafanya kikao cha pamoja na CAG kuhusu taarifa za ukaguzi kwa ripoti inayoishia Juni 2017.
“Yale mambo yote yaliyoibuliwa na CAG kwenye ripoti ikiwamo suala la Sh. trilioni 1.5, CAG alieleza katika taarifa yake hakuna uwiano wa fedha na matumizi ya fedha hizo,” alisema.
Mnyika alisema serikali ilishatoa maelezo kuhusu hilo, lakini CAG aliagizwa aende kufanyia kazi taarifa hiyo na ilipaswa Januari 14, mwaka huu CAG atoe maelezo hayo kwa kamati.
“Ili kukwepesha serikali isiwajibike kwa bunge, Spika akaamua kusambaratisha kamati ya PAC na LAAC na kutangaza hicho alichokiita mgogoro kati ya CAG na Bunge, kama kambi hatukubaliani nalo,” alisema.
Alimtaka Spika kuruhusu kamati hizo kufanya kazi zake kama zilivyopangwa.
“Hivi kama CAG anaitwa tarehe 21 ni kitu gani kilimfanya Spika kusitisha shughuli za kamati hadi tarehe 25, kwanini asingesubiri hadi tarehe 21 halafu akasema kutokana na kilichotokea tumeamua hivi, kitendo hiki kinaashiria katika mawazo ya Spika tayari ameshafanya uamuzi kabla ya Kamati ya Maadili kumshauri,” alisema.
Hata hivyo, alisema kikao cha Bunge kitakachoanza Januari 29 miongoni mwa majukumu ni kupokea taarifa za kamati katika utendaji wake wa mwaka mmoja.
“Sasa mnafahamu hapo katikati Kamati za Bunge za PAC na LAAC zilitoa maagizo mengi kwa serikali ikiwamo suala la Lugumi, tunaona hili nalo linakwenda kufunikwa, pia lipo suala jingine la ufisadi wa chanjo mbalimbali fedha hazikupelekwa kwa halmashauri, pia kashfa ya magari 777 ya Jeshi la Polisi ilitakiwa kufanyika uchunguzi wa kijinai,” alisema.
“Kutokana na kamati hazitapata fursa ya kukutana na ofisi ya CAG ili kuandaa taarifa ya kina na kuwasilisha bungeni, tutatumia kila njia za kibunge na Spika asitulazimishe kutumia haki zetu za kikanuni na kikatiba,” alisema.
Alisema kwa kanuni ya Bunge ya 137 inampa fursa ya mbunge mmoja miongoni mwao kupeleka hoja bungeni ya kumwondoa Spika.
Msemaji huyo alisema kambi hiyo inamtaka Spika kuruhusu kamati kufanya kazi zake kabla Januari 25, mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alisema anaungana na maoni ya kambi hiyo.
Post a Comment