Rafiki wa Jay Z alivyojaribu kuchepuka na Beyonce, kilichompata
Jinamizi la unyanyasaji wa kingono wa wasichana wadogo linalomsakama Mfalme wa RnB, R Kelly limeibua mengi na kufukua makaburi yaliyosakafiwa kwa saruji. Na moja kati ya makaburi yaliyofukuliwa ni la simulizi la uhasama kati ya Jay Z na rafiki yake kipenzi aliyejaribu kuchepuka na Beyonce Knowles.
Mtayarishaji wa muziki aliyewahi kufanya kazi na Roc-A-Fella, Choke No Joke amefunguka kuwa Damon ‘Dame’ Dash ambaye ni mmoja kati ya waasisi wa lebo hiyo aliingia kwenye mgogoro mkubwa na Jay Z enzi hizo, alipojaribu kumzunguka akitaka kuchepuka na Beyonce miaka takribani 18 iliyopita.
Choke alifunguka kwenye mahojiano na Empressive akieleza kuwa baada ya Jay Z kushtukia mchezo, alikasirika na kumpiga marufuku Dame Dash kumsogelea Bey. Kwa lugha ya mtaa, wakati huo Bey alikuwa bado ‘ni kisu kikali cha kukatia kucha.’
Mtayarishaji huyo wa muziki aliyafukua hayo akiwa kwenye harakati ya kujenga hoja akikubaliana na maelezo aliyoyatoa DJ Funkmaster Flex kuhusu uhusiano kati ya Jay Z na marehemu Aaliyah akiwa msichana mdogo.
Flex alidai kuwa sio tu R Kelly ambaye alichomoka na Aaliyah akiwa na umri mdogo (miaka 15) bali hata Jay Z aka Hov ana hatia hiyo.
Lakini Flex akagusia kuwa Dame Dash pia alimzunguka Jay Z wakati huohuo naye akajilambia mtoto Aaliyah kisirisiri.
Jay Z na Dame Dash wakiwa na Aaaliyah kwa nyakati tofauti
Kwa mujibu wa Choke, Jay Z aligundua usaliti huo wa Dash kwa Aaliyah ndio maana alimkurupusha mapema alipoanza kumsogelea Bey siku za baadaye.
Hata hivyo, Choke alidai kuwa tofauti na Aaliyah, Beyonce hakumruhusu Dash kutimiza lengo lake nyuma ya pazia.
“Beyonce hakutaka kumsaliti Jay kwa namna ile. Wote tunafahamu ilifikia hatua pale Roc-A-Fella ambapo Dame hakuwa anaruhusiwa kabisa kumsogelea Beyonce. Kila mmoja aliyefanya kazi pale wakati ule alifahamu,” Choke alifunguka.
“Lakini kama nilivyosema, Beyonce hakutaka huo uchafu. Na sababu hasa iliyofanya Aaliyah akubali huenda ni kwa sababu walifanya kama siri na kujitahidi kuitunza,” aliongeza.
Hata hivyo, ingawa Jay Z hajajibu madai hayo, Dash amejitokeza kukanusha akimponda Flex.
“Flex ni mfano wa jinsi mtu mjinga alivyo. Na unatakiwa kumpata mtu mjinga ili kuonesha mfano wa jinsi gani mtu mwenye akili alivyo,” alisema Dash.
Lakini ukweli ni kwamba pamoja, Dash na Jay Z waligeuka kuwa maadui wakubwa siku za usoni, uadui ambao umedumu kwa miongo.
Sababu ya kubadilika kwa mambo kutoka urafiki wa damu wa biashara hadi uadui mkubwa hazijawahi kufahamika vizuri zaidi ya tetesi nyingi na majibu ya jumla kuwa ni mgongano wa kimaslahi. Of-course, kwa namna ambavyo Beyonce alijaaliwa kuwa maslahi haswaaa (mashallah) ni lazima ingetokea mgongano wa kuleta cheche zinazochochea na kutibua migogoro mingine iliyowasha moto wa uadui.
Jay Z, Dame Dash na Kareem ‘Biggs’ Burke walianzisha Roc-A-Fella Records mwaka 1995, wakijichanga na kukung’uta mifuko kufanikisha ndoto yao.
Ukitaka kujua urafiki wao ulikuwa wa damu na biashara, walishirikiana kwa pamoja kuwezesha utayarishaji wa albam ya kwanza ya Jay Z ‘Reasonable Doubt’. Kwa maana hiyo, Dash ana mchango wa kipekee katika mafanikio ya muziki wa Jigga tangu akiwa 0. Awali, Jay Z alihangaika kutafuta lebo ya kusimamia kazi zake lakini kila alikobisha hodi alikataliwa, akaona bora kukusanya nguvu na marafiki wa kweli tuisukume ndoto yetu.
Inawezekana tamaa ya tunda la bustani ya Eden ‘Malkia Bey’ wa enzi za Destiny’s Child, yaani yule Beyonce aliyekuwa mbichi, ilimchanganya Dash, mate yakamjaa akaamua kuuweka rehani urafiki wa damu!
Huenda hicho nacho kilichochea pamoja na mambo mengine kubadili urafiki huo kuwa chuki kali kati ya Jigga na Dash waliotweta pamoja wakitoa jasho na damu kuisimamisha .
Beyonce na Jay Z walikutana mwaka 1997, kwa mujibu wa Beyonce alipoulizwa mwaka 2007, na wakati mwingine alieleza kuwa alipokutana na Jigga alikuwa na umri wa miaka 18.
Penzi lao lilianza kuonekana hadharani mwaka 2001. Na mwaka 2002 wakalikoreza rasmi na kuwa ‘penzi na kazi’ ambapo waliachia ngoma yao ya kwanza ‘03 Bonnie & Clyde’.
Leo, Beyonce ana umri wa miaka 37, mama wa watoto watatu anayeunda umoja wa wanandoa (couple) wanamuziki wenye nguvu kubwa zaidi duniani. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana za Forbes, hii ni familia bilionea ikiwa na utajiri wa $1.25 bilioni (Beyonce $355milioni & $900 milioni).
Lakini mwaka 2016, liliibuka bomu lingine ambalo limebaki kuwa kama tetesi, kuwa Jay Z alichepuka na mwanamitindo Rachael Roy ambaye aliwahi kuwa mke wa ndoa wa Dame Dash (walioana mwaka 2005 wakaachana 2009). Na ikadaiwa kuwa Beyonce alimuimba kwa hasira kwenye ‘Sorry’ iliyopatikana kwenye albam ya ‘Lemonade’ akimtaja kama ‘Becky with the good hair’.
Wakati drama ya Jay Z kuchepuka na Rachael ikiendelea, Dash alijitokeza akidai kuwa Jay Z na Beyonce ni ‘waoga’ kwa kushindwa kujitokeza hadharani kukanusha tetesi hizo. Lakini hata yeye Dash alisema hana uhakika kama Jay alipita mama mtoto wake huyo ambaye wakati huo walikuwa wameshaachana. Ilibaki hivyo, tetesi zikaishia kama tone la barafu kwenye moto.
Kama madai ya Flex na Choke ni ya kweli, mafanikio haya ya maisha ya ndoa leo yangekuwa ndoto ya alinacha kama Beyonce angejaribu kumlambisha Dash asali ya Jigga.
*Ni hivi, usikubali kuonjwa na ‘rafiki mtu’, baki kwenye mzinga baraka zitakufuata.
*Na usijaribu kuvunja urafiki kwa uzuri wa shemeji, kuna maisha yako; kuna kesho.
Chukua hiyo.
GPL
Post a Comment