0
DR Congo: Watu 900 wameuawa katika vita vya kikabila
Vita vya kikabila magharibi mwa Jmahuri ya Kidmeokrasi ya Congo vimesababisha vifo vya takriban watu 890 katika muda wa siku tatu mwezi uliopita, Umoja wa mataifa unasema.

"Duru za kuaminika" zinaeleza mapigano kati ya jamii za Banunu na Batende yalizuka katika vijiji vinne huko Yumbi, ofisi ya Umoja wa mataifa kuhusu haki za binaadamu inasema.

Nyumba 465 na majengo yaliteketezwa au kuharibiwa, zikiwemo shule mbili za msingi, kituo cha afya, soko na ofisi ya tume huru ya uchaguzi katika eneo hilo, Umoja huo umesema.

Raia walioachwa bila ya makaazi ni pamoja na watu 16,000 waliotafuta hifadhi kwa kuvuka mto Congo hadi katika nchi jirani ya Congo-Brazzaville, umeongeza.

"Ni muhimu kwamba ghasia hizi za kushtusha zichunguzwe kwa haraka na kwa kina na watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria," amesema kamishna wa haki za binaadamu katika Umoja wa mataifa, Michelle Bachelet.

Takriban watu 82 walijeruhiwa katika shambulio hilo, kwa mujibu wa ripoti, lakini Umoja wa mataifa umesema unatarajia idadi ya walioathirika kuongezeka.

Ripoti zinaashiria mapigano yalizuka wakati watu wa kabila la Banunu walipojaribu kumzika mojawapo ya viongozi wao wa kitamaduni katika ardhi ya kabila la Batende.

Uchaguzi wa urais katika eneo hilo pamoja na katika maeneo ya Beni na Butembo mashariki mwa jimbo la Kivu kaskazini, uliahirishwa hadi Machi huku tume ya uchaguzi ikieleza ni kutokana na ukosefu wa usalama na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Post a Comment

 
Top