0
Hatima ya Akina Mbowe na Wenzake Kujulikana Leo
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, leo watafika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ukamilishaji wa masharti ya dhamana waliyopata mwishoni mwa wiki iliyopita.

Machi 27, Mbowe na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa nane, ombi lao la dhamana likaahirishwa uamuzi kwa siku mbili ili Hakimu akajiridhishe.

Alhamisi, Hakimu Wilbard Mashauri alikubali ombi la dhamana licha ya washitakiwa kutokuwepo mahakamani siku hiyo kutokana na gari la kuwatoa mahabusu ya Gereza la Segerea kuharibika.

Mbali na Mbowe (56), washitakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (52), Mbunge wa Kibamba John Mnyika (37), Mbunge wa Musoma Mjini, Esther Matiko (41), Katibu Mkuu, Vincent Mashinji (45) na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu (39).

Hakimu Mashauri alisoma masharti ya dhamana kuwa ni washtakiwa kujidhamini kwa hati ya maneno ya Sh. milioni 20, wadhamini wawili kwa kila mshtakiwa wanaotoka taasisi zinazotambulika watakaosaini hati yenye thamani hiyo ya fedha.

Aidha, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Mbowe na wenzake kukaa gerezani kwa siku saba.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu katika Barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Shtaka la tatu, ilidaiwa katika siku ya tukio la kwanza katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinodnoni, Mbowe wakati akiwahutubia wakazi wa Kinondoni, alitamka maneno ya uchochezi kuwa "Ninapozungumza hapa kiongozi wetu wa kata ya Kinondoni Hananasif yupo mochwari... Amekamatwa na makada wa CCM kwa msaada wa vyombo vya ulinzi na usalama... Wamemnyonga, wamemwua halafu sisi tunaona ni jambo la kawaida... Tunacheka na polisi... Tunacheka na CCM", alinukuliwa kwamba alitoa maneno hayo ya kuleta chuki na uchochezi kwa Watanzania.

Pia shtaka la nne ambalo ni kosa la uchochezi na kusababisha chuki miongoni mwa jamii, Jamhuri imedai Februari 16, mwaka huu katika mkutano wa umma uliofanyika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Mbowe alifanya uchochezi na kusababisha chuki kinyume na sheria kwa kutamka yafuatayo:

"Tumejipa kibali cha kutangulia mbele ya haki... haiwezekani wanaume wazima na akili zetu na wake zetu na watoto wetu tukafanywa ndondocha.. hii ni nchi ya ajabu. Mimi leo nipo hapa kulinda taifa... kule Afrika Kusini Jacob Zuma amelazimishwa kujiuzulu... Robart Mugabe wa Zimbabwe kang'olewa, kang'olewa Waziri Mkuu wa Ethiopia... juzi ameondoka kwa people's power. Magufuli ni mwepesi kama karatasi".

Katika shtaka la tano la uchochezi wa uasi linalomkabili Mbowe peke yake, inadaiwa katika tarehe na maeneo hayo, alihutubia mkutano wa hadhara akiwa na nia ya kupandikiza chuki na dharau kwa Watanzania dhidi ya uongozi wa kisheria uliopo madarakani kwa kusema "Nitaongoza mapambano nchi hii kwasababu tumechoka kuuawa... matokeo ya Watanzania 100 watakaokufa wataleta haki katika taifa hili. Wangapi wapo tayari kuchukua bei hiyo?"

Katika shtaka la sita la uchochezi wa uasi, wakili Nchimbi aliendelea kudai, katika tarehe hiyo hiyo na maeneo hayo mkoani Dar es Salaam, Mbowe alitoa matamshi ya kupandikiza chuki na dharau kwa upande wa raia wa Tanzania dhidi ya mamlaka halali kuwa; "Hii nchi inadharaulika... imejengewa misingi wa uwoga, kwa lugha nyingine wanaume ni kama mademu, si unawaona hao wanavaa suruali, waoga, bure kabisa... juzi ametekwa kijana wetu, wanasema yupo mochuari, haki ya Mungu ingekuwa nchi nyingine Kinondoni ingekuwa majivu... Lissu amepigwa risasi machine gun na vyombo vya dola... Watanzania mnarudi nyuma... kuna mwandishi wa habari leo ana siku 86 amebebwa na vyombo vya dola... suluhu ya nchi hii haipo bungeni. Suluhu ya nchi hii ipo kwa wananchi wenyewe... lakini ili tupate suluhu hiyo... ni lazima tukubali kubeba majeneza... Inawezekana leo mnaogopa kufa... Ni bora tuwabebe wachache hata wakiwa 200 waliokufa katika ukombozi ili hatimaye nchi hii isimame kama nchi ya wanaume wengine katika dunia hii".

Katika shtaka la saba la kushawishi kutendeka kwa kosa la jinai , inadaiwa katika tarehe hiyo hiyo na maeneo hayo, Mbowe alishawishi wakazi wa Kinondoni kutenda kosa la kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali.

Katika shtaka la nane la kushawishi utendaji wa kosa la jinai, linalomkabili mshtakiwa wa pili Msigwa, ilidaiwa katika maeneo hayo hayo Msigwa alishawishi raia na wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.

Post a Comment

 
Top