Wanaume na vijana ni waoga na wameanza kurudi nyuma katika harakati za kisiasa.Hivyo ndivyo anavyodai Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee.
Mdee aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani akidai wanaume wamekuwa waoga na wameanza kurudi nyuma.
Maadhimisho hayo yamefanyika nchi nzima kwa wanawake katika sekta mbalimbali kutoa misaada kwa wenzao waliolazwa katika hospitali mbalimbali nchini, kufanya usafi, kuwatembelea wazee na yatima.
Katika maadhimisho hayo, mawaziri mbalimbali wanawake walishiriki makongamano na kutoa kauli za kuhimiza usawa wa kijinsia na maendeleo kwa wanawake.
Akizungumza jijini Mbeya katika maadhimisho hayo, Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe aliwataka wanawake kusimama na kuonyesha uwezo wao katika kupigania demokrasia kwa vitendo.
“Kwa sasa vijana wanarudi nyuma, hivyo wanawake ndio kimbilio la mabadiliko ya kweli katika nchi, tusimame kidete tusife moyo, tupambane kwa vitendo dhidi ya dhuluma ya kidemokrasi inayotoweka katika nchi yetu,” alisema Mdee.
Alisema wengi wanaohama vyama vya upinzani na kujiunga na CCM, wakiwamo wabunge na madiwani ni wanaume na kusema kuwa hizo ni dalili za woga.
Alisema hakuna kitu chochote kinachohitajika kwa sasa katika Taifa kama Katiba mpya hivyo kuwataka Watanzania bila kujali itikadi, ukabila, dini ama rangi zao wapaze sauti zao kuidai akisema ndiyo itakayokuwa suluhisho.
Wanawake MCL wamliza mke wa Azory Gwanda
Katika kuiadhimisha siku hiyo, wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), walimtoa machozi Anna Pinoni, mke wa Azory Gwanda walipomtembelea nyumbani kwake Kibiti mkoani Pwani.
Azory, ambaye alitekwa na watu wasiojulikana Novemba 21, 2017 katika mji wa Kibiti alikokuwa anaishi na kufanya kazi hadi jana alikuwa hajapatikana.
Pamoja na mambo mengine, wanawake hao wa MCL walimpa bima za afya kwa ajili ya matibabu ya watoto wake wawili, mmoja akiwa amezaliwa hivi karibuni, wakati Azory akiwa ameshatoweka.
Walimkabidhi pia misaada mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya Sh700,000.
Anna alijikuta akibubujikwa machozi na kushindwa kuzungumza alipoona kundi la wafanyakazi wanawake wa MCL, likiwasili nyumbani kwake kuungana naye katika kuadhimisha siku hiyo.
“Sijui niseme nini, mwenzenu nashindwa hata cha kuongea, mmekuwa wema sana kwangu hasa wakati huu ninapopitia kipindi kigumu... sina cha kuwalipa zaidi nawashukuru,” alisema.
Awali, kiongozi wa msafara wa wanawake hao wa MCL, Lilian Timbuka alisema upendo, umoja na mshikamano ndio uliowasukuma kuadhimisha siku hiyo pamoja na Anna.
“Tunajua mwenzetu upo katika kipindi kigumu, lakini tukutie moyo na shime kwamba usichoke kupiga goti na kumuomba Mungu na sisi tupo nyuma yako tunaendelea kukuombea upate nguvu,” alisema Lilian.
Mama Janeth Magufuli
awasifu wanawake wa Dar
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli aliupongeza Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuanzisha vikundi zaidi ya 400 vya wanawake vinavyojishughulisha na usindikaji mazao, ushonaji na uchoraji.
Pia aliupongeza mkoa huo kwa kuwa na vikundi vya kukopeshana (Vicoba) vipatavyo 2,748 ambavyo kwa pamoja, vina mtaji wa jumla ya Sh10.4 bilioni
“Ni imani yangu kuwa mikoa yote na taasisi nyingine za kiserikali na kiraia zitaiga mfano wa Dar es Salaam katika kuwawezesha wanawake kiuchumi,” alisema.
Mawaziri wanawake
walivyoadhimisha
Akiwa mkoani Rukwa, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliwaonya wakurugenzi watendaji wa halmashauri nchini wasiotenga asilimia nne ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya mikopo ya wanawake.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa Nelson Mandela, Waziri Ummy alisema atachukua majina ya wakurugenzi wasiotenga fedha hizo na kuyakabidhi kwa Rais John Magufuli ili awachukulie hatua za kinidhamu ikiwamo kuwaondoa katika nafasi zao.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema Rais Magufuli ana imani na utendaji wa wanawake ndio maana amewateua kwenye wizara nyeti kama vile elimu, afya na madini akiamini kwamba watafanya kazi kikamilifu kuleta maendeleo ya nchi.
“Tunafanya jitihada kuboresha elimu hapa nchini. Tunaangalia pia elimu ya juu, tunashirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha mfumo wa elimu hapa nchini,” alisema Profesa Ndalichako.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema usawa wa kijinsia unaoonekana katika elimu ya msingi na sekondari utatoa matokeo chanya katika elimu ya juu.
Akizungumza katika kongamano la sita la Wanawake Wenye Mafanikio Tanzania (TWA) lililofanyika jijini Dar es Salaam katika alisema ili wanawake wapige hatua, wanahitaji kuwa na uelewa wa kutosha ambao bila shaka ni elimu.
Katika hatua nyingine, Serikali imewapiga marufuku wanaume wanaotumia mali za familia kama dhamana za mikopo bila kuwashirikisha wake zao.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fabian Daqarro ameyasema hayo jana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Daqarro alisema wapo wanaume wanaotumia mali za familia kama nyumba kukopa bila kuwashirikisha wake zao na wakishindwa kulipa mikopo, mali ya familia hupigwa mnada.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment