0
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mtwara Bw. Stephen Mafipa  kumtafuta popote alipo na kumkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi Bw. Fortunatus  Kagoro  kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha.

Mbali na Bw. Kagoro pia Kaimu Mweka Hazina Bw. Heri Hamad Afisa Mipango Bi Teresia Nsumba  nao ameagiza wakamatwe na baada ya uchunguzi watakaobainika kwamba hawajahusika na ubadhilifu huo watarudishwa kazini. "Lazima fedha za Serikali zitumike kama ilivyokusudiwa."

Watendaji hao wanadaiwa kutumia sh. bilioni 1.8 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa kuchora mchoro na kujenga msingi katika maeneo mawili tofauti.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Februari 26, 2018) wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Masasi na Halmashauri ya wilaya ya Masasi akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara.

Amesema mwaka 2014  Serikali ilipeleka sh milioni 575 wilaya Masasi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri hiyo na fedha hizo ziliishia kutumika  katika hatua za maandalizi ya awali ikiwa ni pamoja na kutengeneza michoro ya jengo.

Waziri Mkuu amesema 2016/2017 Serikali ilipeleka tena sh. bilioni 1.25 kwa ajili ya ujenzi huo, ambapo Halmashauri hiyo ilienda kutafuta eneo lingine na kufanya tena shughuli zilizokuwa zimefanyika na kuanza ujenzi ambao umeishia katika msingi na fedha zimeisha.

Pia amewataka watendaji hao kutotumia fedha za makusanyo ya ndani kwa ajili ya kuziba pengo la fedha za mradi huo ambazo baadhi yake hazijulikani zilipo na amewaagiza Madiwani kutoruhusu jambo hilo.

"Madiwani msikubali kutumia fedha za makusanyo ya ndani kupeleka kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo ambayo tayari Serikali ilishatoa fedha ya ujenzi wake.

Amesema Serikali inahitaji kuona fedha za maendeleo zinazopelekwa katika Halmashauri mbalimbali nchini zinatumika kama ilivyoelekeza na si vinginevyo na Serikai haitakuwa na mzaha kwa mtumishi atakayezitumia vibaya.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 26, 2018.

Post a Comment

 
Top