Ray C Atoa Sababu Kumtomzika Ruge Mutahaba
VUNJA ukimya! Sexy lady wa Bongo Fleva, Rehema Yusuf Chalamila ‘Ray C’ ametaja sababu ya kutomzika Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba ‘Jasiri Muongoza Njia’, Risasi Jumamosi lina habari kamili.
Kama ulikuwa hujui, mlezi mkuu wa Ray C kimuziki na kimaisha kwa jumla alikuwa Ruge hivyo kifo chake hakiwezi kuwa ni jambo dogo kwa staa huyo wa Wimbo wa Na Wewe Milele.
Ruge alifariki dunia Februari 26, mwaka huu nchini Afrika Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kusumbuliwa na matatizo ya figo kwa miezi kadhaa kisha kuzikwa kijijini kwao, Kiziru-Kabale, Bukoba mkoani Kagera, Machi 4, mwaka huu.
RAY C HAKUONEKANA
Msiba wa Ruge uligusa na kuhudhuriwa na watu wengi wa kada mbalimbali wakiongozwa na Rais John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mawaziri na viongozi wengine huku wasanii wakiwa kama wote isipokuwa mwanadada Ray C. Wasanii wengi waliopitia mikononi mwa Ruge waliibua gumzo msibani, lakini Ray C hakuonekana.
MINONG’ONO MINGI
Kutoonekana kwa Ray C msibani kuanzia jijini Dar hadi kule Bukoba kuliibua minong’ono mingi kwa mashabiki wake wakitaka kujua kulikoni kwani wanajua Ruge alikuwa sawa na baba yake.
RAY C AELEZA SABABU
Katikati ya minong’ono na sintofahamu hiyo ya kutoonekana kwa Ray ndipo gazeti hili likajipa kazi ya kumtafuta mwanamuziki huyo almaarufu Kiuno Bila Mfupa ambaye alifunguka sababu ya kushindwa kufika kwenye msiba wa Ruge.
Katika mazungumzo yake na Gazeti la Risasi Jumamosi akiwa kwenye makazi yake jijini London, Uingereza, Ray C alisema wakati msiba huo unatokea alikuwa safarini kwenye ziara ndefu ya kimuziki nchini Marekani.
NI MSIBA MZITO
Ray C alisema kuwa, pamoja na kwamba ulikuwa ni msiba mzito kwake na kwamba alijikuta akitokwa machozi kutokana na uchungu wa kumpoteza mtu wake huyo wa karibu, lakini alishindwa kuahirisha au kuvunja ziara zake kwani alishalipwa kwa ajili ya shoo za watu. “Iliniuma sana, tena sana na mpaka sasa hivi inaniuma, natokwa na machozi kwa kumpoteza mtu muhimu kwangu.
“Nakumbuka wakati ninapata taarifa za msiba nilikuwa Marekani kwenye tour (ziara) kwa ajili ya shoo na nilishalipwa. “Kiukweli sikuwa na jinsi kwani nilishindwa kabisa kukatiza ziara,” alisema Ray C ambaye baada ya shoo za Marekani ataendelea na ziara yake nchini Ufaransa na Sweden.
WARAKA WA RAY C KWA RUGE
Siku chache kabla ya kifo, Ray C alimwandikia Ruge waraka mzito akimtaka kuamka kitandani alikolazwa ili amwambie kinachoendelea maishani mwake. Kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Instagram, Ray C alimwandikia Ruge;
“Amka bwana, nimeshachoka kusubiri, meseji zangu hujibu, simu hupokei, nina stori kibao nataka kukwambia ingawa najua utanichamba, lakini nilishazoea kukwambia kila kitu changu kinachoendelea kwenye maisha yangu. “Tunagombanaga mpaka tunablokiana, lakini tukionana tu, tukaangaliana, tunabaki kucheka tu. “Nilishazoea kukwambia mambo yangu kwa sababu we’ ndo’ msiri wangu. We’ ndo’ unanipaga makavu nikiharibu.
“Kuna muda mpaka ninalia na ukiona ninalia, ndo’ unazidi kunipa makavu bila huruma. “Ninaondoka kwa hasira ingawa moyoni ninajua uliyoniambia ni kweli… ninakununiaaa ila haifiki wiki, huyo nimeshakuja ofisini kwako.
“Muda mwingine sina hata cha maana cha kukwambia ila nakuja tu ofisini kukuona unitanie nicheke! “Ray C umenimiss eeh… Kama nywele hujazielewa unanipa live Ray C nenda katoe hizo nywele.
“Nikikuona tu ninapata amani ya moyo. Nikitoka tu studio wa kwanza kukutumia demo! Ni wewe, wewe tu miaka yote tangu nimeanza muziki kwa sababu ninaheshimu sikio lako na ninaliamini.
“Mwezi wa ngapi sasa huu Ruge! Natuma meseji, ninakupigia, natamani kukuimbia japo kidogo upate nguvu sikupati…Ruge najua huko ulipo unaumia sana, najua unataka kuamka na kufanya kazi zako. Please wake up (tafadhali amka) babaa.
“Please! You are too strong (tafadhali wewe ni imara sana) babaa. Don’t give up please for you (usijikatie tamaa mwenyewe).
“Nishike mkono. Nibusu shavuni. Vyovyote vile. Nakupenda (wimbo unaoupenda sana). Amka Ruge.” Hata hivyo, pamoja na waraka huo mzito wa Ray C, lakini Ruge ambaye pia alikuwa meneja wa mwanadada huyo hakuamka hadi Mungu alipomchukua mja wake.
RAY C NI NANI?
Ray C aliyezaliwa Mei 15, 1982 mkoani Iringa ni mwimbaji wa R&B, Afro-Jazz na Taarab ambaye mkononi ana albamu nne za Mapenzi Yangu (2003), Na Wewe Milele (2004), Sogea Sogea (2006) na Touch Me (2008).
Ray C aliyesifika kwa kukata mauno alianza kujulikana baada ya kutoa nyimbo kadhaa kama vile, Sikuhitaji, Mapenzi Yangu, Na Wewe Milele, Ulinikataa na nyingine nyingi zilizompa umaarufu. Awali alikuwa mtangazaji wa Radio East Africa kabla ya kwenda Clouds FM na hatimaye kuwa mwimbaji maarufu aliyeutingisha na anayeendelea kufanya poa kwenye muziki wa Bongo Fleva
Post a Comment