0
Kesi ya Halima Mdee: Mahakama yaelezwa kuhusu ushahidi
Upande wa utetezi katika kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe Halima Mdee umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa imebaki miezi 4 kesi hiyo kufikisha miaka miwili huku ikiwa haijamaliza kusikilizwa.

Hayo yameelezwa na Wakili wa Mdee Hekima Mwesipu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuuc Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali, Dasy Makakala kuomba kesi iahirishwe.

Wakili Makakala amedai shauri hilo lilikuwa kwa wakili mwingine na bado hajalipitia hivyo anaomba ahirisho. Wakili Mwesipu amedai kuwa kesi hiyo imeacha miezi 4 kufikisha miaka miwili huku ikiwa usikilizaji wake haujaisha, hivyo anaomba ahirisho la mwisho.

Baada ya kusema hayo Hakimu Simba ameutaka upande wa mashitaka kuhakikisha tarehe ijayo kesi hiyo inasikilizwa  na kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 16, 2019. Katika kesi hiyo tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wamekwishatoa ushahidi katika kesi hiyo akiwamo  mkuu wa Kituo cha Polisi cha Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP) Batseba Kasanga.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Julai 3,2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) iliyopo mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni,  Mdee anadaiwa kutamka maneno dhidi ya  Rais John Magufuli kuwa  “anaongea hovyohovyo , anatakiwa  afungwe breki”  na kwamba kitendo ambacho kingeweza  kusababisha uvunjifu wa amani. Mdee alifikishwa mahakamani hapo Julai 10, 2017 na yupo nje kwa dhamana.

Post a Comment

 
Top