0
Kasi ya ujenzi SGR, yaikuna Kamati ya Bunge
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), unaoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa KM 300 na kusisitiza kuwa Bunge litaendelea kupitisha fedha za mradi huo hadi utakapokamilika kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Moshi Kakoso, aliyasema hayo eneo la Soga mkoani Pwani baada ya kamati hiyo kukagua na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa katika mradi huo na kusisitiza kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuusimamia kwa ukaribu zaidi ili mradi uweze kukamilika kwa wakati.

"Kamati imekagua mradi na imeridhika na hatua za ujenzi wa reli hii, hivyo hakikisheni unakamilika kwa viwango vinavyokubalika na ukabidhiwe mwishoni mwa mwaka huu kama mkataba unavyoelekeza,” alisema Kakoso.

Aidha, aliipongeza serikali kwa jitihada zinazoendelea kufanyika, kampuni ya ujenzi na wataalamu wote wanaosimamia ujenzi wa reli hiyo kwa kuwa kazi nzuri ya usanifu imefanyika, ambapo kwenye baadhi ya madaraja magari yatapita chini na reli itapita juu na mengine reli itapita chini na magari yatapita juu.

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, Jafari Michael, ambaye ni Mbunge wa Moshi Mjini, aliishukuru serikali kwa hatua kubwa za ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo kwa kuwa inapita katika mikoa sita yenye uzalishaji mkubwa wa mazao na chakula na pia itakuza uchumi wa nchi kwa kupata mizigo kupitia nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Naibu Waziri anayeshughulikia Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, alisema kazi ya ujenzi wa tuta la reli umefikia asilimia 64 na miundombinu ya reli hiyo ishalazwa kwa zaidi ya kilomita 40.

Mhandisi Nditiye alitoa wito kwa wananchi kuitunza miundombinu ya reli kwa sababu inajengwa kwa kutumia fedha nyingi na ni urithi kwa vizazi vijavyo na faida kwa taifa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iko katika ziara ya kutembelea na kukagua miundombinu inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Dodoma.

Post a Comment

 
Top