0
Kimenuka! Wanamuziki wawili wakubwa wa Afro-Pop kutoka Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul Jumaa ‘Diamond Platnumz’ na Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ yamewakuta nchini Kenya, Amani limeinyaka.  Wasanii hao wakali wamepata pigo baada ya Serikali ya Kenya kupitisha maamuzi mazito ya kupiga marufuku moja ya nyimbo zao kuchezwa au kuimbwa nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoenea mapema wiki hii nchini humo, Serikali ya Kenya ilipiga marufuku wimbo wao maarufu wa Kwangwaru ambao Diamond ameshirikishwa na Harmonize ambao umekamata vilivyo Kenya.

Taarifa ya Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Kudhibiti Filamu Kenya (KFCB), Ezekiel Mutua ilieleza kuwa bodi hiyo haitaruhusu watoto kuimba wimbo huo kwa maelezo kuwa una lugha ya mafumbo ambayo yanapotosha.

MBALI NA KWANGWARU

Mbali na Kwangwaru, Mutua alionya kwamba Serikali ya Kenya itapiga marufuku muziki wa kigeni na matamasha yanayochochea tabia mbaya, kuhujumu utamaduni, desturi na sheria za Kenya.

“Dansi na disko zitadhibitiwa ili kuhakikisha wanamuziki wa kigeni hawaji Kenya kwa wingi kuharibu heshima, utamaduni na desturi zetu,” alisema Mutua. “Kwa nini wanacheza muziki ambao umepigwa marufuku katika nchi zao?” Alihoji Mutua.


Mutua alikwenda mbele zaidi na kuwaonya walimu wakuu nchini humo kwa kuwataka kutoruhusu wanafunzi kuimba Wimbo wa Kwangwaru. Alisema walimu wakuu watakaoruhusu wanafunzi kuimba wimbo huo wataripotiwa Wizara ya Elimu ili wachukuliwe hatua kali.

INAMA…INAMA…

“Haitakuwa kama zamani, wanamuziki wa kigeni wanakuja nchini kwetu kuharibu utamaduni wetu, watoto wanaimbia mama zao ‘inama…inama’ na hata wakiwa shuleni. “Huo wimbo (Kwangwaru) una maana mbaya, tumeupiga marafuku,” alisema Mutua.

SHOO MARUFUKU

Akizungumza wakati wa mkutano na wachezaji katika Hoteli ya Mombasa Beach jijini Mombasa, Kenya, Mutua alisema Serikali itafanya kuwa vigumu kwa watu ambao maudhui yao yamezuiliwa katika nchi zao kufanya kazi (shoo) nchini Kenya.

Mbali na hilo, Mutua alisema wanamuziki wamekuwa wakikataa kulipa kodi ya Mamlaka ya Mapato ya Kenya. “Wanashirikiana na klabu na kulipa moja kwa moja kwa nchi zao za asili hivyo hawalipi kodi. “Wao wanakuja hapa, wanarukaruka kama mashujaa na supastaa kisha wanafanya ya kwao wanaondoka na fedha moja kwa moja kwa nchi zao za asili,” alisema Mutua.


MSISITIZO

Bosi huyo wa KFCB alidai KRA (Mamlaka ya Mapato ya Kenya) itaanza kuweka msisitizo ambapo wasanii wa kimataifa wanaofanya shoo kwa kushirikiana na wamiliki wa taasisi au kumbi za starehe watatakiwa kukatwa kodi za Serikali.

Mutua alisema KFCB itashirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani kuweka uratibu wa Serikali ya kitaifa ili kuhakikisha kanuni zinatekelezwa. “Watu wanaomualika Diamond na watu wengine kufanya shoo hapa kwa kutumia maudhui ambayo yamezuiwa Tanzania na nchi nyingine yoyote, hatutakubali.

“Tutawabana ili kuzuia mchakato wa kukimbia kodi kwa sababu taasisi au klabu zinapoingia mikataba na wasanii kama Diamond huwa wanaweka pesa zote mfukoni moja kwa moja bila kulipa kodi ya Serikali. Hiyo ni rushwa,” aliongeza Mutua. Afisa huyo alisema kuwa watoto wadogo wanapaswa kulindwa kutokana na maudhui yaliyofichika.

BASATA WATOA NENO

Akizungumzia sakata hilo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza aliliambia Amani kuwa, waliona ishu hiyo kwenye makundi ya mitandao ya kijamii, lakini halijawafikia rasmi. Hata hivyo, aliongeza kuwa kama kuna jambo kama hilo, wasanii ndiyo wanapaswa kuwajulisha Basata baada ya kuwa wamepokea taarifa rasmi kutoka taasisi husika.

FELA AFUNGUKA

Amani pia lilizungumza na mmoja wa mameneja wa Wasafi, Said Fela ambaye alisema hawana taarifa za jambo hilo na hawawezi kuamini habari za mitandaoni kwani mitandao mingine huwa inaandika chochote ili kujipatia umaarufu.

WIMBO WA KWANGWARU

Kwangwaru ndiyo wimbo ambao umesikilizwa na kutazamwa zaidi kwa Afrika Mashariki ukiwa na zaidi ya watazamaji milioni 42 kwenye Mtandao wa You Tube na kwa nchini Tanzania haujawahi kufungiwa.

Post a Comment

 
Top