0


Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif, ametangaza rasmi kujiunga na chama cha ACT Wazalendo yeye pamoja na wafuasi wake ili kuendeleza mapambano waliyokuwa wakiyafanya kupitia chama cha CUF.

Maalim Seif ametangaza maamuzi hayo Leo March 18, 2019 ikiwa ni muda mfupi kupita baada ya Mahakama kuu Kanda ya Dar es Salaam Kuhalalisha Uenyekiti wa Profesa Lipumba ndani ya CUF.

"Sasa tumeamua kuwa sasa imetosha, mapambano ya kisiasa lazima yaendelee, tumeamua kutafuta jukwaa la kufanyia siasa ambalo ni ACT -Wazalendo" Amesema Maalim Seif  wakati akitangaza kujiunga na chama cha ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam 

Maalim Seif ameendelea kusema; "Nimetumia muda mrefu sana kuijenga CUF, nimepata taabu sana kuiacha CUF, lakini namshukuru Mungu naendelea na safari, tumeamua kuutupa mzigo wa CUF ili kusalimu roho zetu.

"Kabla ya kuchukua maamuzi haya tulitembelea baadhi ya vyama ili kuwaambia, ikitokea sisi kuhama mko tayari kutukaribisha? lakini kwenye masharti tulivyochambua tukaona ACT Wazalendo masharti yao hayakuwa magumu.

"Sasa hivi sisi hatutaki malumbano na watu, sasa kama wanataka kwenda kuchukua ofisi zao waende wakachukue lakini kwa taarifa tu ofisi nyingi za CUF ni za watu binafsi na lililobaki sasa ni wao na wenye majengo yao. 

''Kuhusu wabunge wa CUF wanaotuunga mkono, bado ni wanachama wa CUF, hilo tumewaachia wao kama wataamua kujiunga na ACT-Wazalendo ni wao, kama wataamua kuendelea huko pia ni sawa, sisi hatuna maamuzi juu yao.

“Hatua tunayochukua leo ya kuhamia ACT-Wazalendo ni ya kihistoria. Umma haujawahi kushindwa dunaiani kote. Na umma wa Watanzania hautashindwa. Shusha Tanga Pandisha Tanga Safari iendelee,”  Amesema Maalim Seif.

Post a Comment

 
Top