0
Wavaa Bimini Katika Ofisi za Imma Kukiona Serikali Kuanza Msako
Ikiwa zimepita siku chache baada ya Mhe. Rais John Magufuli kuzungumzia mavazi yenye staha, tayari Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa kushirikiana na Kamati ya Uadilifu ya Ofisi hiyo, imeanza kufuatilia utekelezaji wa waraka wa mavazi kwa watumishi .


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Februari 7, 2019 na kitengo cha mawasiliano serikalini wizarani hapo, ofisi hiyo haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote wa umma watakaobainika kukiuka waraka huo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa ofisi hiyo imeanza utekelezaji wa Waraka wa Mavazi Namba 3 wa mwaka 2007 kwa watumishi wa ofisi hiyo kwa lengo la kujiridhisha na kiwango cha utekelezaji wake.

Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Ukuzaji Maadili, Sehemu ya Ufuatiliaji Uzingatiaji wa Maadili, Janeth Mishinga, amesema ofisi hiyo ndiyo msimamizi wa miongozo ya kiutumishi ikiwamo kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma.

Pia taarifa hiyo imesema kuwa kanuni ya kwanza inaelekeza utoaji wa huduma bora na kuongeza kuwa moja ya kigezo cha watumishi wa umma kutoa huduma bora ni pamoja na kuvaa mavazi yenye staha.

“Ukaguzi uliofanywa katika Ofisi ya Rais-Utumishi umebaini kuwa asilimia 95 ya watumishi wameonekana kutekeleza waraka huu wa mavazi ikiwamo kuwahi kazini na asilimia tano ya watumishi waliobainika kutoutekeleza waraka wamekumbushwa kuuzingatia,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, Mishinga katika taarifa hiyo, alitoa wito kwa wasimamizi wa taasisi zote za umma nchini kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa waraka huo na kuwahimiza watumishi walio chini yao kuwahi kazini.

Hivi karibuni, Rais Magufuli, alizungumza na viongozi wa dini Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo alisema inafahamika kuwa watu wasiovaa mavazi ya heshima hawaruhusiwi kuingia kanisani, lakini itakuwa vyema kama watu hao hawataruhusiwa kuingia sehemu yoyote.

“Najua Roman Catholic wanaweka matangazo kuwa wenye nguo zisizo na heshima hawaruhusiwi kuingia kanisani, sasa tuende mbali na hapo, tusizungumze tu wasiruhusiwe kuja kanisani, wasiruhusiwe mahali popote, ndio maana nafurahi kanisa la mzee Kakobe wanafunga na vitambaa wote,” alisema Rais Magufuli siku hiyo.

Post a Comment

 
Top