MUUGUZI wa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha, Martin Chama amesimamishwa kazi ya kutoa huduma za uuguzi na ukunga kwa mwaka mmoja na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha baraza hilo cha 196 baada ya kumtia hatiani kwa makosa mawili kati ya manne yaliyowasilishwa katika baraza hilo Septemba mwaka jana na aameanza kuitumikia adhabu hiyo tangu Februari 7, 2019.
Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Agnes Mtawa ameyataja makosa hayo kuwa ni kufika kazini akiwa amelewa na kutaka kuhatarisha usalama wa wagonjwa na ndugu zao kwa kushindwa kutoa huduma kwa umakini na weledi.
“Awali ofisi ya msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga ilipokea tuhuma kutoka Hospitali ya Mount Meru Arusha kupitia kwa muuguzi mkuu wa mkoa ambaye pia ni msimamizi wa maadili wa mkoa wa Arusha kwa mujibu wa sheria N0 1 ya mwaka 2010,” amesema.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa za awali Septemba 29 Chama alikuwa zamu ya usiku majira ya saa tatu usiku alifika kazini akiwa amelewa.
Akiwa amelewa Chama anadaiwa alianza kuwasumbua ndugu waliokuwa wakiwaangalia wagonjwa wao kutaka kuendelea kutoa huduma kwa wagonjwa ili hali akiwa amelewa sana hali ambayo ingeweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa kwa kuwa hakuwa na umakini. Mtawa amesema tuhuma hizo ziliwasilishwa na walalamikaji wawili waliokuwa wakiuguza wagonjwa wao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment