0
Mali za Vigogo Waliokopa SUMA JKT Kuanza kupigwa Mnada
Watu mbalimbali waliokopa matrekta Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), wakiwamo wabunge na mawaziri, sasa matumbo joto baada ya serikali kutangaza mali zao kukamatwa na kupigwa mnada.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema jana bungeni jijini hapa kuwa shirika hilo limepanga kuuza kwa mnada wa mali za vigogo waliokopa matrekta katika shirika hilo.

Dk. Mwinyi alisema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Ruth Mollel, alilouliza kwa niaba ya Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka.

Aidha, alisema tangu Rais John Magufuli kuagiza wakopaji wa matrekta kulipa madeni yao, jumla ya Sh. bilioni 2.9 zimekusanywa.

Dk. Mwinyi alisema SUMA JKT imeziandikia mamlaka za ajira za viongozi waliokopa ambao mpaka sasa hawajalipa mikopo yao, wakiwemo wabunge, wakuu wa wilaya na mikoa.

Katika swali lake, Mbunge huyo alitaka kujua mkakati wa kukusanya madeni ya fedha zilizokopwa katika idara mbalimbali kutoka SUMA JKT na wale waliokopa matrekta huku akitaka watangazwe magazetini.

Akijibu swali hilo, Waziri huyo alisema SUMA JKT lilikopesha idara zake Sh. bilioni tano na mpaka sasa Sh. bilioni mbili zimelipwa sawa na asilimia 45.

“Tunaamini fedha hizi zitalipwa kutokana na kuwa idara zilizokopa zinafanyia biashara,” alisema.

Alisema Sh. bilioni 2.9 zimekusanywa na wanajipanga kupiga mnada mali za waliokopa ambao watashindwa kulipa madeni yao katika kipindi hiki cha kukusanya madeni.

“Tayari orodha ya wadaiwa sugu wa matrekta ilishatolewa na kwa sasa wameziandikia mamlaka za ajira kwa viongozi wakiwamo wabunge ambao mpaka sasa hajalipa madeni haya,” alisema.

Dk. Mwinyi alisema orodha ilishatolewa kwenye vyombo vya habari na Spika alishakabidhiwa orodha ya wabunge wanaodaiwa.

Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Bulembo, alitaka kuwekwa orodha ya viongozi wa serikali wakiwamo wabunge na kutangaziwa ili wafahamike.

Awali, katika swali la msingi, Kaboyoka alisema SUMA JKT idara ya zana za kilimo ilikopesha Sh. 5,355,153,000 kwa idara mbalimbali.

“Taarifa ya CAG za mwaka zimeonesha kuwa hadi Juni 30, 2016 ni kiasi cha Sh. 534,785,000 ambayo ni chini ya asilimia 10 ndicho kimerejeshwa, Je, ni kiasi gani hadi sasa kimerejeshwa kwenye idara ya zana za kilimo?” alihoji.

Alihoji pia serikali itakubaliana naye kwamba uzembe wa kutohakikisha mikopo ya fedha za serikali inarudishwa kwa wakati ili wakulima wengine nao waweze kukopeshwa kumechangia kukwamisha juhudi za kupunguza umasikini Tanzania.

“Serikali inachukua hatua gani kuwawajibisha waliohusika na utoaji huo wa mikopo bila kuhakikisha inarudishwa kwa wakati,”alihoji.

Akijibu maswali hayo, Dk. Mwinyi alisema hadi Januari 31, mwaka huu, Sh. 2,389,082,000 zimerejeshwa na Sh. 2,966,071,000 bado hazijarejeshwa.

Post a Comment

 
Top