0
Katibu Mkuu CCM: Tundu Lissu Anaumwa Ugonjwa wa Deko na Kiburi
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), anaumwa ugonjwa wa deko huku akimuomba Rais Dk. John Magufuli aanze kutibu ugonjwa huo.

Kauli hiyo aliitoa juzi wilayani Kilosa mkoani Morogoro, katika ziara yake ya kazi ikiwa ni sehemu ya maadhimino ya miaka 42 ya kuzaliwa kwa CCM.

Dk. Bashiru alidai Lissu amekuwa akisema uongo katika nchi za Ulaya huku akiota siku moja atakuwa Rais wa Tanzania.

Wakati mtendaji huo wa juu wa CCM akiyasema hayo, Lissu amekuwa akiendelea na ziara yake katika nchi za Ulaya.

Kwa sasa yupo Marekani akieleza kile alichodai hali ya demokrasia nchini na kupigwa kwake risasi.

Dk. Bashiru alidai dalili za ugonjwa wa aina ya Tundu Lissu ni kusema uongo, dharau, deko, uonevu, kiburi, majivuno.

“Ila shukrani ya punda ni mateke. Namuomba Rais wetu (Dk. John Magufuli) aanze kutibu ugonjwa wa deko unasomesha watu wanazunguka kutukana nchi yao na Rais wao kisa ugonjwa wa deko.

“Yupo msomi mmoja anaitwa Tundu Lissu ameugua ugonjwa wa deko, anadeka hajui jembe kwa maisha yake, hajui mpunga unalimwaje wala samaki wanavuliwaje.

“Hajapanda bodaboda muda mrefu na watoto wake hawasomi shule hizi anazunguka dunia nzima kutuchafua.

“Tunao Tundu Lissu wengi Serikalini tumewaamini tumewapa dhamana ila ukiwatembelea ofisini wanadeka, mara nyingine hawapo, wanajipendelea wao,” alisema Dk. Bashiru na kuongeza:

“Ugonjwa huu unaambukizwa na tumeulea na wauguzi na madaktari wa ugonjwa huu ni Watanzania nyie wenyewe. Huu ugonjwa hatari, unaambukizwa ni hatari kuliko Ukimwi.

Anasema tumeweka Kifungu kwenye Katiba ya CCM cha kuzuia watu kugombea urais siyo kweli ni uongo”.

Dk. Bashiru alisema dalili za ugonjwa huo wa deko ni ubinafsi, kuota urais wa Tanzania kuwa na kiburi na kwenda Ulaya kuzungumza lugha za wakoloni lakini sasa anayemwita dikteta amefuta mashamba kwa ajili ya wanyonge.

“Nilipomskiliza nikasema ni muongo na kwa sababu anaumwa ugonjwa unaitwa Tundu Lissu, basi yupo kwenye hali mbaya.

“Ugonjwa wa Tundu Lissu ni hatari ila unaponyeka, amuache Rais (Dk. John Magufuli) atumikie wanyonge.

“Watendaji wote wa serikali ambao hawataki kupona ugonjwa huu watafute serikali nyingine, ajira ni hiyari waandike barua waseme chama hiki hakipendi dhurlma, mimi nadhulumu, hakipendi uongo mimi muongo, uachie madaraka,” alisema.

Post a Comment

 
Top