0


DAR ES SALAAM: Penzi la mastaa wa Afrika Mashariki, mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na mtangazaji nyota wa Radio NRG ya jijini Mombasa nchini Kenya, Tanasha Donna Oketch, linaendelea kuibua mapya kila uchwao, safari hii mjadala mzito ni kuhusu wawili hao kuzaa, Ijumaa linakupa zaidi. 



Fukuto la Tanasha kuzuiwa kuzaa na Diamond au Mondi, limeibuka katika kipindi hiki ambacho tetesi za mrembo huyo kuwa ana ujauzito wa Mondi zikiwa zinaendelea kusambaa kwa kasi ya moto wa petroli.



Diamond ambaye ukali wake kwenye Bongo Fleva unatishia amani ya wanamuziki wengine kwenye kilinge hicho, rekodi yake ya kuwa kwenye uhusiano na watoto wazuri inaharibiwa na kutofanya uamuzi wa kuoa na kuwa na mke halali wa ndoa. Itakumbukwa hivi karibuni hasimu wake mkubwa kwenye muziki, Ali Saleh Kiba ‘Alikiba’ aliandika historia kwa kumuweka ndani mtoto mzuri, Aminah Khaleef kutoka pande hizohizo za Pwani ya Mombasa, jiji linaloongozwa na Gavana Hassan Joho.



Lakini safari hii Mondi ambaye sifa yake kubwa ni kurudisha alichopata kwa mashabiki wake, amekaririwa mara kadhaa akisema kuwa kwa mrembo huyo chotara wa Kiitaliano na Kikenya amefika na kwamba “lazima amuweke mtoto ndani mwaka huu”. Awali, Mondi aliahidi kumuoa Tanasha ifikapo Februari 14, mwaka huu katika Sikukuu ya Wapendanao, lakini baadaye akasema amesogeza mbele hadi tarehe atakayoitangaza baadaye.

KUTOKA MOMBASA

Habari za moto kutoka Mombasa zinaeleza kuwa, familia ya Tanasha imekaa kikao kizito na kuweka maazimio muhimu kuhusu binti yao huyo huku kubwa likiwa ni kumtaka mrembo huyo asizae na Mondi. Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya familia ya Tanasha, kimezungumza na Gazeti la Ijumaa kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini na kuanika ukweli wa kila kitu kuhusiana na ishu hiyo.



Akizungumza kwa tahadhari huku akisisitiza asitajwe kabisa gazetini, ndugu huyo alianza kwa kusema: “Yapo mengi, lakini familia kwa sasa imesisitiza Tanasha asizae na Mondi. Tumejadiliana mengi kama familia…hadi tumefikia uamuzi huo, ni kwamba tumechambua mengi.” Anaendelea kusema: “Kwanza lazima ujue kuwa Tanasha anatoka familia ya watu walioshika dini sana. Wazazi wake ni waumini wazuri wa Dini ya Kikristo na hawapendi mambo yasiyofuata utaratibu.”



KWA NINI ANAZUIWA?

Chanzo chetu kinatiririka kwamba, familia haina tatizo kabisa na binti yao kuwa katika uhusiano na Mondi kwa sababu “akipendacho mtu chake” lakini katika suala la kuzaa lazima utaratibu ufuatwe kwanza.



“Sisi hatuna shida na mapenzi yao, lakini hatutaki mambo ya kutuharibia binti yetu kisha amuache. Msimamo wa familia huku Mombasa ni kwamba, kama kweli Mondi anampenda Tanasha, taratibu zote zifuatwe kwanza, wafunge ndoa ndipo wazae,” alisema na kuongeza: “Tumesema hivyo kwa sababu ya historia ya huyo Diamond, kwa mfano aliwahi kuwa na Wema Sepetu (staa wa Bongo Muvi) kwa muda mrefu, lakini walikuja kuachana. Akaenda kwa Zari (Mganda Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’) akazaa naye watoto wawili.



“Zikasikika taarifa kuwa wataoana, lakini hapakuwa na kitu kama hicho, badala yake ikaja kugundulika kuwa kumbe alizaa na Hamisa Mobetto (mwanamitindo) akiwa ndani ya uhusiano na Zari. “Sasa kwa tabia na mwenendo huo, hatuwezi kumuamini moja kwa moja kwamba anaweza kumuoa mtoto wetu, mpaka pale atakapofika nyumbani rasmi na kukamilisha mambo yote ya kimila kisha wafunge ndoa, ndiyo mambo ya kuzaa yafuate.”

Mwanafamilia huyo anamalizia kwa kusema: “Nasisitiza tena, sisi familia hatuna tatizo na wao kupendana, maana ni uamuzi wao, ila tunataka ndoa kwanza kabla ya kuanza kuzaa. Unadhani akimzalisha, halafu akamuacha, atakuwa mgeni wa nani? Ndiyo maana wazee hawataki kusikia hivyo.”

MAMA DIAMOND HUYU HAPA

Gazeti la Ijumaa liliwasiliana na mama mzazi wa Mondi, Sanura Kassim na kumuuliza kama anafahamu chochote kuhusiana na madai hayo, akasema anachojua ni kwamba wamemuasa Mondi atulize mpira kwanza. “Hayo mambo unayosema umeyapata kutoka Mombasa hatuyajui, lakini sisi kama familia tumekaa na Nasibu (Mondi) na tumemshauri kwa sasa atulie kwanza, aache mambo ya kuzaa. Lakini zaidi ongea na Esma (Khan) atakuambia zaidi,” alisema mama Mondi.

Gazeti la Ijumaa lilizungumza na Esma ambaye ni dada wa msanii huyo. Kitu cha kwanza Ijumaa lilimhoji kuhusu tetesi za Tanasha kuwa na mimba ambapo Esma alisema: “Weee! Weee! Weee! Mimba? Hakuna kitu kama hicho, Tanasha hana mimba.” Ingawa Esma alisema hawana taarifa za ndugu wa Tanasha kumzuia binti yao kuzaa na ndugu yao, lakini msimamo wa familia yao unafanana na ule wa familia ya kina Tanasha.

“Hayo ya Mombasa sijayasikia kwa kweli, lakini sisi tumemketisha Mondi na kuzungumza naye. Kwamba kwa sasa atulie kwanza, afanye muziki na kula bata na mchumba’ke Tanasha. Kama ni watoto anao, tena wa jinsia zote, hana haja ya kuwa na haraka. Ana watoto wawili wa kiume na wa kike mmoja,” alisema Esma.

Watoto wa Mondi ambaye anatesa na Ngoma ya Tetema aliyopiga kolabo na Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ ni Tiffah Dangote na Prince Nillan aliozaa na Zari ambaye kwa sasa anaishi nchini Afrika Kusini na Prince Dyllan (Abdul) aliyezaa na Mobeto.

TANASHA ATAHADHARISHWA

Uhusiano wa Mondi na Tanasha umekuwa gumzo mitandaoni na Afrika Mashariki nzima huku mijadala mikali ikiibuka kila wakati kuhusu Mondi kumuoa mrembo huyo au kumuacha kama historia inavyoonesha huko nyuma kwa warembo wanaopita mikononi mwake. Mchangiaji mmoja mtandaoni alimtahadharisha Tanasha kuhusu kuzaa na msanii huyo kabla ya ndoa, akimtaka aangalie kilichotokea kwa Zari.

Aliandika: “Kama ni kiu ya watoto, Zari alimzalia watoto wawili na bado hakuridhika, akaenda kwa Mobeto. Awe makini, waingie kwenye ndoa kwanza kabla ya kufikia uamuzi wa kubeba mimba.”

Mara kadhaa Shehe Mkuu wa Dar es Salaam, Sheikh Alhadi Mussa Salim, amepata kumshauri msanii huyo kuangalia nyendo zake na kufikiria suala la kuingia kwenye ndoa kama imani yake ya Kiislam inavyomwelekeza.

Imeandikwa na Joseph Shaluwa na Imelda Mtema

Post a Comment

 
Top