Serikali ya Tanzania na Japan kupitia Shirika la Maendeleo la nchi hiyo (JICA) zimesaini mkataba wa Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Gerezani lengo likiwa kupunguza adha ya msongamano jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini humo kabla ya Hafla ya utiaji saini mkataba huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alisema mradi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Serikali ya Awamu ya Tano wakati ikiomba ridhaa ya kuongoza kwa wananchi na kwamba iliahidi kutekeleza ujenzi wa miundo mbinu imara nchi nzima.
“ Rais John Magufuli anatekeleza ahadi alizowaahidi wananchi, utiaji saini huu inaonyesha wazi Serikali ina mahusiano mazuri na mataifa mengine hata wahisani wana imani na fedha wanazozitoa zinavyotumika,” alisema Waziri Kamwelwe.
Alibainisha kuwa Serikali iko makini katika uboreshaji wa miundo mbinu katika sekta zote ikiwemo usafiri wan chi kavu, angani na majini na kusisitiza ujenzi huo ukikamilika utapunguza adha ya foleni na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Waziri Kamwelwe alisema kuwa bado Serikali inaendelea na ujenzi wa miundo mbinu ikiwemo ya Ujenzi wa Reli ya umeme( Standard Gauge), viwanja vya ndege, madaraja na barabara.
Kwa uapnde wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mhandisi Patrick Mfugale alisema mradi huo unatarajiwa kujengwa kwa miezi 24 huku gharama zake zikiwa Sh bilioni 22.48 hadi kukamilika kwake na mkandarasi msaidizi Sh bilioni 2.600.
Mhandisi Mfugale alifafanua kuwa ujenzi wa mradi huo ni sehemu mkakati ya kupunguza msongamano huku akibainisha Kampuni ya Sumitomo Mitsui Construction (SMCC) ndio imepewa jukumu la ujenzi.
Katika hatua nyingine, alisema daraja hilo litakuwa na urefu wa mita 40, upana wa sentimeta 30.4 na njia sita za watembea kwa miguu.
Wakati huo huo, Mhandisi Mfugale alisema Tanroads itahakikisha mkandarasi na mhandisi wanajenga daraja hilo kwa weledi na kukamilisha ndani ya muda.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu wa JICA nchini, Toshio Nagase alisema utiaji saini mkataba wa mradi huo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Shirika hilo, Shinichi Kitaoka alipotembelea nchini mwaka 2017.
Nagase alisema ana imani mkandarasi aliyekabidhiwa atajenga daraja kwa bora a hali ya juu hata kuliko Daraja la Mfugale.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundo Mbinu, Selemani Kakoso alisema kukamilika kwa daraja hilo kutawasaidia wananchi kuwahi kazini muda wa asubuhi na wakati kurudi nyumbani.
Ameiomba Serikali kutoa fursa kwa wakandarasi wazawa kushiriki kwenye miradi ya ujenzi kwani kuna uthibitisho unaonyesha wakipewa wanafanya kazi kikamilifu akitolea mfano Ujenzi wa Daraja la Mto Mara na Ujenzi wa Meli Ziwa Nyasa na Mwanza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment