Mfanyabiashara Henry Munisi (30), mkazi wa jijini Mbeya, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka ya kuchapisha taarifa za uongo kwa njia ya mtandao kumwita Rais Dk.John Magufuli mwizi.
Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally. Alisomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita.
Katika mashtaka hayo, Mwita alidai kuwa Desemba 28, mwaka jana jijini Mbeya, alichapisha taarifa za uongo kuhusu Rais.
Upande wa Jamhuri ulinukuu taarifa hiyo kupitia ukurasa wa Facebook wa Munisi kwamba, "Jinsi Magufuli alivyochota Sh. trilioni 1.5 za ATCL akitumia ujanja wake wa kuleta ndege ili atuibie," alinukuliwa taarifa hiyo. Mshtakiwa alikana mashtaka hayo.
Hakimu Ally alimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za taasisi ya kuaminika watakaotia saini hati ya dhamana ya Sh. 500,000 kila mmoja.
Hata hivyo, alishindwa kutimiza masharti hayo na amerudishwa rumande mpaka Februari 6, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment