0

ZAIDI ya watuhumiwa 11,000 wa dawa za kulevya wamekamatwa nchini tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, bunge lilielezwa jana mjini hapa.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, aliyasema hayo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mwantumu Dau Haji.

Mavunde alisema tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo, watuhumiwa 11,071 wameshakamatwa na kwamba kati ya hao, 3,486 ni wafanyabiashara wa dawa za kulevya na tayari wamefikishwa mahakamani.

Katika swali lake, Mbunge huyo alitaka kujua mpango wa serikali wa kuhakikisha inarejesha kasi ya kupambana na Dawa za kulevya.

"Kazi ya kushughulikia wimbi la dawa za kulevya nchini imekuwa ya kusuasua na kutoridhisha. Je, serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inarejesha kasi ya kupambana na dawa hizo?" alihoji mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Mavunde alisema idadi hiyo  ni ya watuhumiwa waliokamatwa hadi Februari, mwaka huu, ikiwa ni takribani mwaka mmoja sasa tangu kuundwa kwa chombo hicho Februari, mwaka jana, baada ya bunge kutunga sheria mpya ya kudhibiti na kupambana na dawa hizo namba 5 ya mwaka 2015.

"Kutokana na kuongezeka kwa kasi ya kupambana na dawa za kulevya imesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa matumizi ya dawa hizo nchini,"alisema Mavunde.

Alisema mamlaka hiyo imepewa nguvu kisheria za kukamata, kupekua, kuzuia mali na kuchunguza mashauri yote ya dawa za kulevya na makosa mengine yanayohusiana nayo ikiwamo mali zitakazothibitika kupatikana kutokana na biashara ya dawa za kulevya.

Aidha, alisema Zanzibar imekuwa ikitumiwa kama uchochoro wa kupitisha dawa hizo na kwamba vimekuwapo na vikao vya kutengeneza mfumo wa udhibiti katika eneo hilo.

Mavunde alitoa wito kwa wabunge kushiriki kikamilifu juhudi za serikali za kupambana na dawa za kulevya kwa kuwa madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo,  yanaathiri wote ikiwamo kuongezeka vitendo vya uhalifu na matumizi ya serikali katika kuwahudumia waathirika.


Post a Comment

 
Top