0
WIZARA ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, imesema serikali haijaruhusu majahazi kubeba abiria kutokana na usalama mdogo na ukosefu wa vifaa vya uokozi vya mawasiliano.

Naibu Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na usafirishaji, Mohamed Ahmada, aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake, Suleiman Sarhani, aliyetaka kujua tatizo la usafiri Pemba linatatuliwa vipi.

Ahmada alisema kwa mujibu wa Sheria za usafiri baharini zinazoratibiwa na Mamlaka ya Usafiri Majini (ZMO), vyombo vilivyotengenezwa kwa kutumia mbao ikiwamo majahazi ni marufuku kubeba abiria.

''Mheshimiwa Naibu Spika nataka kutoa taarifa kwamba serikali bado haijaruhusu majahazi kubeba abiria kutokana na usalama mdogo na ukosefu wa vyombo vya kisasa vya uokozi,' 'alisema.

Alisema majahazi mengi hadi sasa hayana vifaa vya kisasa vya mawasiliano ya redio pamoja na vifaa vya uokozi wakati yanapotokea majanga ya ajali baharini.

Alisema serikali inafahamu licha ya kupiga marufuku majahazi kuacha kubeba abiria, lakini wapo manahodha wanaokaidi agizo hilo la kisheria .

''Hivi karibuni nimeshuhudia mwenyewe huko Tanga jahazi limepata ajali na kuzama huku abiria wakipoteza maisha ikiwamo watoto,' 'alisema.

Alisema wizara imeanza ukaguzi wa vyombo hivyo katika maeneo ya bandari Unguja na Pemba na kuona kwamba vinatekeleza agizo la serikali la kuacha kubeba abiria

Post a Comment

 
Top