0

Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam imepitisha silingi bilioni 75 za bajeti kwa mwaka 2018/2019 huku kipaumbele kikiwekwa kwenye utalii.

Ndani ya bajeti hiyo zimetengwa fedha kwa ajili ya kununua mabasi makubwa ya kitalii ambayo yatakuwa yakizunguka katika viunga mbalimbali vya Jiji la Dar es Salaam kuwazungusha watalii.

Meya wa jiji hilo, Isaya Mwita alisema tayari mabasi mawili yameshawasili na yanasubiriwa mengine ili biashara ya utalii ndani ya jiji ianze mapema iwezekanavyo.

“Nadhani madiwani kwa pamoja tumeona imefika wakati kuweka nguvu kubwa kwenye utalii katika jiji letu kama ilivyo katika miji mingine mikubwa barani Afrika mfano majirani zetu Mombasa na Lamu,” alisema.

Mjumbe wa baraza la madiwani la halmashauri hiyo na mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea alisema ni hatua kubwa kwa jiji na ilipaswa kuwa hivyo muda mrefu.

“Ukitembea katika nchi mbalimbali wenzetu wamezingatia mno suala la utalii wa ndani ya mji, naweza kusema tumechelewa ilitakiwa tufike huko muda mrefu ndiyo sababu suala hili lilipokuja kwetu tumeliridhia,” alisema.

Post a Comment

 
Top