Padri Raymond Mayanga wa Parokia ya Yohane Mbatizaji Luhanga amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kumsaka mtu aliyempiga risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafishaji (NIT), Akwilina Akwilini, kumweka wazi ili awaombe radhi Watanzania.
Akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa mwanafunzi huyo inayofanyika katika viwanja vya NIT, Mabibo, Padri Mayanga amesema mtu huyo hata akifungwa miaka 30 hadi 40, Akwilina hatarudi.
“Awe amefanya kwa nia nzuri au mbaya vyombo vinavyohusika vikimaliza taratibu zake kama ni kupitia televisheni ama nini huyu mtu aombe msamaha, vinginevyo hatutafika mbali. Leo kwa Akwilina huenda kesho kwa mwingine,” amesema.
Naye mwakilishi wa familia ya Akwilina, Aloyce Shirima amesema, “Tunaomba mtufikishie salamu kwa Rais John Magufuli kuwa wale wote waliofanya kitendo hicho wachukuliwe hatua stahiki. Taifa haliwezi kuendelea kwa kuondokewa na wasomi kizembe.”
“Akwilina ni mtoto wa sita katika familia ya watoto nane wa mzee Akwilini na ni mtoto pekee aliyependa elimu katika familia hiyo.”
Rais wa Serikali ya wanafunzi NIT, Mchunja Othman amesema, “Alikuwa mcheshi asiyejua kununa. Tunaiomba Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha inalisimamia hili ili haki itendeke. Hii inatupa fursa ya kujifunza sisi kama binadamu maisha yetu siyo ya kudumu hivyo tutende mema.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment