0
Kampeni za Ubunge katika jimbo la Kinondoni kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA zimefunguliwa leo rasmi katika uwanja wa Ali Mapilau ,Mwananyamala na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama hicho akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa kamati kuu, Edward Lowassa.

Chadema imemsimamisha Niabu Katibu Mkuu wake Zanzibar, Salum Mwalimu kugombea jimbo hilo ambalo lilikuwa likishikiliwa na Maulid Mtulia wa CUF ambaye amejiunga na CCM ambayo imemsimamisha tena kugombea nafasi hiyo.

Akizungumza katika kampeni hizo Mbunge wa Arusha Mjini, Gobless Lema alisema muda wa chama hicho kulia umekwisha na kuwataka wanachama na hasa vijana wa Kinondoni kutembea nyumba kwa nyumba kuhakikisha mgombea wao Salumu Mwalimu anaibuka mshindi.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Taifa BAVICHA, Patrick Ole Sosopi alisema, " Mimi kama Mwenyekiti wa Vijana wajanja zaidi Tanzania nitahakikisha tunabeba lawama hadi Mwalimu anatangazwa mshindi, tunawataka Polisi kutuacha tupambane wenyewe na wasiingilie na wakijaribu kumteka kiongozi wetu yeyote na wao tutawateka,"

Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule Profesa Jay licha ya kufanya kampeni hizo kwa kuimba nyimbo zake na wanachama wa chama hicho pia alitumia fursa hiyo kuwaomba wapiga kura wa Kinondoni kuhakikisha hawamchagui Maulid Mtulia kuwa mbunge wao kutokana na usaliti aliowafanyia.

Post a Comment

 
Top