0
Kada wa CCM, Dk Mwigulu Nchemba ameeleza sababu za kuwaomba wapigakura wa Jimbo la Kinondoni kumchagua mgombea ubunge wa chama hicho, Maulid Mtulia.

Dk Nchemba aliyewahi kuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho (Bara), alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika katika Viwanja vya Biafra jijini Dar es Salaam.

Mtulia alijiondoa CUF Desemba 2, mwaka jana hivyo kupoteza ubunge wa jimbo hilo na baadaye alijiunga na CCM ambayo imempitisha kuwania tena kiti hicho katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Februari 17.

Dk Nchemba alikuwa mgeni rasmi katika kampeni hizo ambazo zilikuwa za aina yake licha ya kutokuwapo mjumbe yeyote wa sekretarieti ya chama hicho kama ilivyo kawaida.


Baadhi ya wajumbe wa NEC akiwamo Steven Wasira walinogesha kampeni hizo zilizokuwa na vikundi mbalimbali vya burudani kikiwamo cha TOT.

Dk Nchemba ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alisema mgombea wa CCM ndiye mwenye uwezo wa kutatua matatizo ya wananchi kwa kuwa ilani inayotekelezwa ni ya chama hicho kilichopo madarakani.

Alisema kuchagua mgombea wa upinzani ni kujikosesha maendeleo kwa kuwa hawawezi kuzifikisha hoja za matatizo ya wananchi sehemu husika.

Huku akisindikizwa na vibwagizo vya nyimbo za TOT, Dk Nchemba ambaye pia ni mbunge wa Iramba Magharibi, alisema mgombea wa CCM ana uwezo wa kukutana na viongozi wa Serikali kuzungumzia matatizo ya wananchi tofauti na wagombea wa upinzani.

Alisema uchaguzi utakaofanyika licha ya kuitwa ni mdogo, lakini ni mkubwa kwa CCM na inauchukulia kwa uzito kwa kuwa ni jambo la kitaifa na ina masilahi nao. Alisema baada ya uzinduzi wa kampeni, kila mmoja awe meneja wa mgombea wa chama hicho.

Dk Nchemba alisema kwa kuangalia tathmini ya hali ya siasa, ajenda za kitaifa zinatekelezwa na CCM hivyo kuhoji mtu anabaki upinzani kufanya nini.

Alisema changamoto kubwa kwa mbunge ni kushindwa kutekeleza ajenda aliyowaahidi wananchi, hivyo akiona hana namna ya kutekeleza ni muhimu kuhama.

Wakati Dk Nchemba akiendelea kuhutubia, baadhi ya vikundi vya uhamasishaji navyo vilikuwa vikiendelea kuzunguka kwenye Uwanja wa Biafra kuhamasisha wananchi waliohudhuria mkutano huo.

“Siasa safi ni kuipongeza Serikali inapofanya vizuri, lakini kwa Tanzania Serikali ikifanya jambo jema kabisa mtu wa upinzani akasifia kesho yake ni kikao cha kuulizwa ni kwa nini unasifia na wakati mwingine wapinzani wanafanya kila namna kukwamisha mipango hiyo,” alisema.

Dk Nchemba alisema, “Wengine hata si wawakilishi, juzi mzee kaenda Ikulu kumsalimia, kesho yake kikao, anaulizwa kwa nini ulimsifia Rais.

“Hata bungeni mpinzani anaweza kwenda kwa waziri moja kwa moja, lakini akienda anaulizwa kwa nini ameenda upande mwingine.”

Alisema, “Mtulia aliangalia hasara ya mwezi mmoja na hasara ya miaka iliyobakia akaona bora ya mwezi mmoja ili baadaye awe mbunge bora.”

Dk Nchemba alisema Mtulia amefanya hesabu zitakazomsaidia kuacha kumbukumbu ya uongozi bora jimboni humo.

“Mipango yote inayotengewa fedha ni Ilani, hakuna mwingine mwenye sera au ilani yake atapangiwa fedha, ni sawa na kupigia kura kivuli, ili usipoteze muda wako, mpigie Mtulia mwenye ilani,” alisema.

“Hata uweke lugha nzuri kiasi gani vocha za Tigo haziingii Vodacom, kawaida kabisa unapoteza kura yako, mwenye ilani umemwona ni Mtulia.”

Dk Nchemba alisema kazi inayofanywa na Rais John Magufuli itabakia kwenye historia ya Tanzania.

“Zaidi ya Sh20 bilioni inatumika kupanua Bandari ya Dar es Salaam, mtu akisema anataka kujiunga na historia hiyo kuna kosa gani? Kuna watu wanalalamika vitu vidogo sana vinavyosemwa, ni mpito tu, eti pesa imeisha... Unatumia pesa ili upate pesa,” alisema.

Huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria, alisema “Huwezi kununua ndege, kujenga reli na kupanua bandari halafu fedha ibaki vilevile. Ukimaliza hayo ndiyo unaanza kushughulika na mishahara. Anachotengeza Rais ni kutaka kujitegemea, huwezi kupandisha mshahara kwa mikopo ya kuomba, kwa hiyo hakuna kosa kwa wale wanaokuja kujiunga na historia hii.

“Haiwezekani upeleke mtu ambaye kazi yake ni kutukana tu, hata sala hazikuwekwa kihasara. Zote ni sifa kwanza kabla ya kuomba (akitumia mfano wa sala ya Baba Yetu) ikishakolea ndiyo unapiga mizinga, sasa uchague mtu kazi yake kutukana?” alisema.

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani alisema watazuia vurugu wakati wa kampeni na kuwataka wananchi kufanya kampeni kwa amani na utulivu huku akionya kuwa atakayefanya fujo atashughulikiwa.

Kabla ya kumleta mgombea jukwani kunadi sera zake, Dk Nchemba aliwapokea kwanza wanachama wa Chadema waliojiunga CCM akiwamo aliyekuwa diwani wa Kata ya Kimara, Pascal Manota.

Ikiwa imesalia takribani dakika tano kufika saa 12.00 jioni, Dk Nchemba alimkaribisha jukwaani Mtulia ambaye alianza kujinadi kwa kujiita mjanja kwa kwa kuthubutu kuacha kiinua mgongo bungeni.

Pia alijinadi kwa kuiweka hadharani familia yake wakiwamo mkewe, watoto na mama yake mzazi kwamba hiyo ni tofauti aliyonayo na wagombea wengine.

Akijinadi kwa wananchi, Mtulia alisema alizuia bomoabomoa iliyokuwa ikitekelezwa na Serikali jimboni humo.

Pia, alisema anampenda sana Rais Magufuli na kwamba, alipokuwa mbunge kwa miaka miwili hakuwa na namba (ya simu) ya kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Alisema baada ya kuingia CCM, namba hiyo anayo, hivyo akaomba apewe ubunge ili akawatumikie kwa kumueleza Rais matatizo yao.

Mtulia ambaye kabla ya kuzungumza na wananchi alionyesha kadi yake ya CCM na kitambulisho cha mpiga kura, aliwaomba waliohudhuria mkutano huo kuwa mabalozi wake kwa kumuombea kura.

Akimnadi mgombea huyo, Wasira alisema wakazi wa Kinondoni na maeneo mengine yanayoongozwa na Chadema yalichukuliwa kwa makosa.

Alisema tuhuma kuwa Mtulia ameingia CCM kwa kununuliwa hazina mashiko.

“Alipotoka Nyalandu (Lazaro aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM) nikawa nasubiri kusikia wao walitumia shilingi ngapi kumnunua, lakini kimya,” alisema.

Wasira alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Chadema iliwadanganya wapiga kura jimboni humo kuwa itapeleka mabadiliko lakini haikuwa hivyo.

“Wananchi walidanganywa Mkoa wa Dar es Salaam kwa mabadiliko ya kuzungusha mikononi tu, sasa wamegundua makosa, kule Arusha wamejiondoa madiwani kumi na moja, Longido walijua mapema kwamba wasingeshinda sasa wamejileta Kinondoni, ndugu zangu naomba mtoe kura kwa Mtulia mapema kabisa,” alisema Wasira.

Mwananchi

Post a Comment

 
Top