0
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetoa onyo kwa wadaiwa sugu ambao hawajajitokeza kuanza kulipa madeni yao, kwamba hatua mbalimbali dhidi yao zinatafuata kokote waliko.

Miongoni mwa hatua hizo, bodi hiyo imetaja kuwa ni kuwatoza wadaiwa hao sugu riba ya asilimia kumi katika deni lao na kutumia taarifa zao kuwazuia kufanya safari za nje ya nchi.

Taarifa ya hivi karibuni ya bodi hiyo , imeeleza kuwa wadaiwa hao wa tangu mwaka wa masomo wa 1994/95, wataanza kusakwa kupitia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambaye anawajibika kukagua mali zote za Serikali.

Mbali na CAG, ambaye ana mkono mrefu wa kuwasaka katika ofisi zote za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma, Serikali za Mitaa na katika miradi ambayo Serikali ina ubia na sekta binafsi, pia kampuni binafsi za ukaguzi wa hesabu, zenye mkono mrefu katika sekta binafsi, zitatumika kuwasaka katika kampuni binafsi na asasi za kiraia.

“Jukumu la CAG na kampuni zingine binafsi za ukaguzi wa mahesabu, ni kulazimisha waajiri kuwasilisha taarifa za wafanyakazi wao ambao ni wahitimu wa elimu ya juu na makato ya mkopo waliopewa,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imefanya marejeo ya Sheria ya Bodi namba 9 ya 2004 na marekebisho yake, inayomtaka kila mwajiri kutoa maelezo kwa maandishi kwa bodi, kuhusu mwajiriwa ambaye ni mnufaika wa mkopo huo, ndani ya siku 28 tangu mdaiwa alipoajiriwa.

Hatua
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mdaiwa yeyote wa bodi hiyo atakayeshindwa kulipa deni lake bila sababu za msingi, kwanza atakuwa akikabiliwa na kesi ya madai chini ya kifungu cha 6 C na H cha Sheria ya Bodi ya Mikopo namba 9 ya mwaka 2004.

Mbali na kukabiliwa na kesi hiyo, pia mkopo wake kwa namna unavyochelewa kuanza kulipwa, utakuwa ukijilimbikizia riba ya asilimia 10.

Taarifa hiyo ya bodi imeeleza kuwa mdaiwa huyo taarifa zake zitapelekwa katika taasisi za kumbukumbu ya mikopo zilizo chini ya Benki Kuu (BoT), ambazo zitazuia wadaiwa hao kupata mikopo katika mabenki na asasi zote za fedha.

Mdaiwa huyo pia atazuiwa kupata udhamini wa Serikali katika muendelezo wa masomo yake, lakini pia atazuiwa kujiunga na chuo chochote cha elimu ya juu ndani na nje ya nchi.

Aidha kwa mujibu wa taarifa hiyo, taarifa zao pia zitawasilishwa katika Idara ya Uhamiaji iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na katika ofisi zote za kibalozi, ili wakose kibali cha kusafiri nje ya nchi.

Hasara nyingine watakayokabiliwa nayo wadaiwa hao, ni Tozo ya Kulinda Thamani ya Mkopo (VRF) ya asilimia sita kila mwaka, itakayotozwa kwa kila mkopo, ili wadaiwa watakapoanza kulipa mkopo waliochukua, walipe kwa thamani ya sasa.

Tozo hiyo imelenga kuepuka athari ya mfumuko wa bei tangu mdaiwa aliponufaika, lakini pia kuwezesha urejeshwaji wa deni, uwe na thamani ya kumhudumia mwanafunzi mwingine mwenye mahitaji kwa sasa na baadaye.

Ambao hawajaajiriwa
Taarifa hiyo pia imeonya wadaiwa wanaodhani kuwa kutokuajiriwa ni sababu ya kutolipa mkopo huo, kwamba mkopo huo unatakiwa kulipwa baada ya kumalizika kwa mwaka mmoja tangu mdaiwa alipofanikiwa kuhitimu masomo yake, au mwaka mmoja tangu mhusika alipokatisha masomo yake kwa sababu yoyote.

Aidha, taarifa hiyo imeelekeza watakaojitokeza, kama wameajiriwa, asilimia nane ya mshahara wao wa kila mwezi, itatakiwa kukatwa na kuwasilishwa kwenye Bodi ili kulipa deni husika.

Lakini pia Bodi hiyo imetengeneza utaratibu kwa ambao hawajaajiriwa, kwamba wanaweza kulipa kiasi cha chini cha Sh laki moja kila mwezi katika akaunti za Bodi zilizopo Benki ya Posta yenye namba CCA0240000032; Benki ya NMB namba 2011100205 na Benki ya CRDB namba 01J1028467503.

Deni lenyewe
Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG, hadi Juni 2014, bodi hiyo ilikuwa imewakopesha wanafunzi Sh trilioni 1.8 kuanzia mwaka wa masomo 1994/95 na kati ya fedha hizo, Sh bilioni 51 zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.

Taarifa hiyo ya HESLB imetolewa siku chache kabla ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako  kusitisha ajira ya Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, George Nyatega kwa tuhuma za udhaifu katika fedha za mikopo zaidi ya Sh bilioni 3.2.

Post a Comment

 
Top