0

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema katika vikao vya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo wa kisiasa Zanzibar, walivyofanya na Rais Ali Mohamed Shein, walikubaliana kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) haifai tena kusimamia uchaguzi na kujadiliana kuhusu namna ya kupata tume nyingine inayoweza kufanya kazi hiyo.

Hivyo, ameelezea kushangazwa na kitendo cha Serikali ya CCM kuukubali uamuzi aliouita batili wa ZEC kutaka kufanya uchaguzi wa marudio.

Akizungumza na viongozi wa CUF Mkoa wa Dar es Salaam katika ofisi za chama hicho Buguruni, Maalim Seif alisema hatua hiyo imedhihirisha kuwa viongozi hao hawakuwa na nia njema kwenye mazungumzo hayo yaliyofanyika mara tisa na baadaye kuvunjika bila mwafaka.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo katika mfululizo wa vikao vyake na viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya na majimbo, yenye lengo la kuwaeleza kuhusu uamuzi uliofanywa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio.

Alisisitiza kuwa kitendo cha kufuta uchaguzi uliokamilika na kutangaza tarehe nyingine ya marudio ni batili na kwamba hakuna msingi wowote wa kutangaza kurudiwa.

Alisema waangalizi wote wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi waliridhishwa na uchaguzi huo kwamba ulifanyika kwa amani, ulikuwa huru na haki na kwamba ana matumaini kuwa wataendelea na msimamo wao huo hadi haki ya wananchi wa Zanzibar itakapopatikana.

“Msimamo wa CUF ni kwamba hakitambui kufutwa kwa uchaguzi na kurejea wito wake kwa Tume ya Uchaguzi kukamilisha mchakato wa kujumlisha kura kwa majimbo yaliyobakia na hatimaye kumtangaza mshindi wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Maalim Seif alisema, CCM na viongozi wake wamepoteza dira baada ya kutoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kutokana na kubakwa kwa demokrasia Tanzania na hasa Zanzibar.

Alisema kauli ya Serikali ya kutaka mabalozi wa nchini za nje na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa wasizungumze na viongozi wa vyama vya upinzani isipokuwa kwa ruhusa ya Wizara ya Mambo ya Nje ni kitendo cha aibu.

Amshukia Jaji Lubuva
Maalim Seif alimshutumu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwa kuunga mkono “hoja dhaifu ya ZEC” ya kutaka kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.

Alisema Jaji Lubuva kama anaweza kutenda haki asingekubali matokeo ya urais na wabunge kwa upande wa Zanzibar, kwa vile uchaguzi huo ulifanyika sanjari na ule wa Zanzibar kwa kuwashirikisha wapigakura haohao, daftari hilohilo na vituo vilevile vya kupigia kura.

Akijibu madai hayo, Jaji Lubuva alisema: “Huyu Maalim na (Edward) Lowassa wanataka kutuchanganya, wasimamizi hawakuona dosari katika uchaguzi wa Tanzania Bara, licha ya kwamba kura zilipigwa katika chumba kimoja.”

Aliongeza: “Maalim namheshimu, sipendi kubishana naye, uchaguzi umekwisha, kinachofuata ni watu kufanya kazi ili watu waone matokeo yake mbeleni na kutoa hukumu.” Alisisitiza kuwa Rais Magufuli hawezi kuiingilia ZEC, bali anaweza kuiingilia Zanzibar kama kutakuwa na machafuko kwa kuwa ni Amiri Jeshi Mkuu.

Alisema ni lazima CCM ikubaliane na misingi ya demokrasia ya vyama vingi na kama haiwezi ni bora kurejesha mfumo wa chama kimoja.

Post a Comment

 
Top