JESHI la Polisi mkoani Simiyu, limekumbwa na kashfa nzito, baada ya watuhumiwa watatu wanaokabiliwa na kesi za ujangili na mauaji kutoboa sehemu ya ukuta wa chumba cha mahabusu kisha kutoroka.
Tukio hilo lilitokea Februari 19, mwaka huu katika katika Kituo cha Polisi Meatu wilayani hapa, ambapo watuhumiwa hao waliokuwa chini ya ulinzi wa polisi walichimba shimo na kutoboa tundu walilotumia kutokea.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo, zimeliambia MTANZANIA kuwa watuhumia waliotoroka ni Chiluli Sitta (28), mkazi wa Kijiji cha Mwasunga ambaye anatuhumiwa kwa kesi ya mauaji, Paschal Masanja (18), mkazi wa Sapa na Masanja Ndengule (45) wote wanakabiliwa na kesi ya kukutwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria.
Washitakiwa hao walikuwa wamehifadhiwa katika kituo hicho cha Polisi, wakisubiri kupelekwa katika gereza la mahabusu lililoko mjini Maswa Mkoa wa Simiyu ili kusubiri kesi zao kupelekwa mahakamani.
Chanzo chetu, kinasema askari saba waliokuwa kazini siku ya tukio, wote wanashikiliwa kwa upelelezi zaidi tangu kutokea kwa tukio hilo.
Askari hao, ni D.5582 Koplo Peter (ofisa wa zamu), F9840D/C Hussein CID,G 4806 PC John, G 8602 PC Yassin,WP 11257 PC Khadija, G 8371 PC Adam na H 8410 PC Kher.
Baadhi ya askari Polisi walisema kwamba watuhumiwa hao waliotoroka saa nane usiku wakati wa kutekeleza mikakati yao hiyo, waliumwagia maji ukuta uliojengwa kwa matofali ya saruji na kisha kuutoa kwa kutumia vipande vya chuma vyenye ncha kali zikiwamo nondo.
“Kinachoonekana kuwa hawa watuhumiwa waliingia mahabusu wakiwa na kipande cha nondo kwani inaonyesha wazi kuwa kabla ya ukuta huo kutobolewa waliumwagia maji na kisha kuanza kutoboa kwa kutumia nondo ambapo walipata tundu kubwa na kufanikiwa kutoroka,” alisema mmoja wa askari wa kituo hicho cha polisi ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Baada ya taarifa za kutoroka kwa watuhumiwa hao hali ya taharuki ililikumba Jeshi la Polisi mkoani hapa, ambapo ilimlazimu Kaimu Kamanda wa Polisi, aliyejulina kwa jina moja la Majaliwa, Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, ambaye alijulikana kwa jina moja la Shana kufika katika eneo la tukio na kufanya ukaguzi.
Wengine ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Meatu, Mrakibu Debora Magiligimba na Mkuu wa Kitengo cha Intelejensia, ASP Kyando, ambao walifika na kufanya ukaguzi katika eneo la tukio, ambapo walibaini namna watuhumiwa hao walivyotumia mbinu za kutoboa ukuta na kutoroka.
RPC anena
MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Onesmo Lyanga, ambaye hakuwa tayari kutoa ufafanuzi wa tukio hilo akidai kwamba ana siku moja tu tangu ahamie katika mkoa huo.
“Nipo katika makabidhiano na hivyo siwezi kulizungumzia suala hili hadi nitakapopata taarifa kamili kwa kina,” alisema Kamanda Lyanga.
Hata hivyo alipoulizwa kama alijua kuna tukio hilo, Kamanda Lyanga hakukubali wala kukataa.
IGP Mangu na mabadiliko
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, amefanya mabadiliko ya kimya kimya kwa kumwondoa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Lazaro Mambosasa na kumhamishia Mkoa wa Dodoma.
“Kamanda Mambosasa amehamishwa hapa, kwa kweli hata sisi
tumeona kwenye taarifa zetu za kijeshi hapa haijatangazwa kama ilivyozoeleka,” kilisema chanzo chetu.
Katika mabadiliko hayo, IGP Mangu, amemteua Onesmo Lyanga kuchukua nafasi ya Kamanda Mambosasa mkoani hapa.
Alipoulizwa kuhusu mabadiliko hayo kufanywa kimya kimya, Msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba alisema hiyo ni sehemu ya utendaji kazi wa kila siku ndani ya jeshi hilo.
“Jamani haya ni mambo ya kawaida tu, huu ni utendaji kazi wa kila siku tuna mambo mengi ambayo tunayashughulikia,”alisema Advera.
Majangili walivyoua rubani
Januari 30, mwaka huu watu wanaodaiwa kuwa ni majangili walitungua kwa risasi helkopta ya doria na kumuua rubani wake, Rodgers Gower, ambaye ni raia wa nchini Uingereza katika pori la akiba la Maswa mkoani Simiyu.
Katika tukio hilo ambalo pia lilimjeruhi askari wa wanyamapori, helkopta hiyo mali ya kampuni ya uhifadhi iitwayo Friedkin Conservation Fund ilikuwa katika doria kwenye pori la uwindaji wa kitalii la Mwiba.
Tukio hilo la majangili kutungua helkopta kwa risasi ni la kwanza kutokea katika historia ya uhifadhi nchini na imeelezwa kuwa doria hiyo ilikuwa inafanyika kufuatia milio ya risasi iliyotokea katika eneo hilo, ambapo majangili hao walikuwa wameuwa tembo watatu na kuchukua meno yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment