Maalim Seif, ambaye aligombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25 ambao matokeo yake yalifutwa, pia amesema endapo CCM itasitisha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika siku 36 zijazo, CUF watakuwa tayari kufanya mazungumzo lakini si kwa wakati huu ambao maandalizi ya kupiga kura yanaendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, katibu huyo mkuu wa CUF aliitoa hofu CCM kuwa chama chake hakina ajenda ya kulipiza kisasi.
Matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani yalifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salum Jecha siku ambayo chombo hicho kilitakiwa kumtangaza mshindi, na mwezi uliopita alitangaza Machi 20 kuwa siku ya uchaguzi wa marudio visiwani humo.
Wakati CUF ikipinga vikali kufutwa matokeo na kutangaza tarehe mpya, Serikali imesema kuna nafasi ya kufanya mazungumzo kabla ya uchaguzi wa marudio kwa kuwa kuna muda mrefu wa kufanya hivyo.
Jecha alitangaza uamuzi huo wakati tayari matokeo ya urais ya majimbo 31 yalishatangazwa, na ya majimbo tisa yaliyosalia yalishahakikiwa, huku washindi wa viti vya uwakilishi na udiwani wakiwa wametangazwa na kupewa vyeti vya ushindi.
“Sijui kwa nini CCM wanaogopa sisi tukiongoza?” alihoji Maalim Seif kwenye mkutano huo na waandishi akiwa pamoja na aliyekuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
“Wana wasiwasi gani, kwamba CUF ikiongoza kutatokea nini? Sisi hatuna ajenda ya kulipiza kisasi,” alisema.
Katika mkutano huo, Maalim Seif mbaye pia ni katibu mkuu wa chama hicho alisema kama CCM ina wasiwasi na idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), haina budi kuondoa shaka kwa kuwa idadi kwa pande zote inakaribiana.
“Hawa wanahisi hawatapata uwakilishi mkubwa, lakini mbona miaka yote tunakuwa na idadi isiyopishana ya wawakilishi?” alihoji.
Kuna Vitisho Zanzibar
Katika mkutano huo, Maalim Seif alisema kumekuwapo vitendo vya wananchi kupigwa na vikundi vya watu wasiojulikana.
Alidai wafanyakazi wa Serikali na taasisi zake wameamrishwa kupeleka vitambulisho vyao vya kazi na vya kura serikalini ili vikahakikiwe.
“Hii si mara ya kwanza wafanyakazi wa Serikali kutakiwa kupeleka vitambulisho, sisi tunajua kuwa wanataka wawatishe kuwa watajua nani kapiga kura na nani hajapiga,” alisema na kusisitiza:
“Hii ni kama kitisho cha kuwalazimisha wakapige kura, zaidi hasa hizo ni dhuluma ambazo wananchi wanafanyiwa.”
Kadhalika Maalim Seif alizungumzia uwapo wa watu wanaovaa soksi usoni na kuwashambulia raia, akisema Serikali haijachukua hatua stahiki kudhibiti hali hiyo.
Alisema watu hao ambao wamepachikwa jina la mazombi, wamevamia maeneo kadhaa kama Baraza la CUF, Jang’ombe na yaleambayo yana wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani humo.
“Wanawapiga watu, wanawajeruhi na wanaiba mali, lakini inashangaza sana mambo haya na si Serikali wala polisi iliyochukua hatua,” alisema.
Maalim Seif alisema amezungumza na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuhusu matukio hayo ya uharamia wanaofanyiwa wananchi, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.
Alisema CCM wanatafuta sababu ili machafuko zaidi yatokee visiwani humo wapate kisingizio.
Aliwataka wafuasi wa CUF kuvumilia hali hiyo ili nchi isiingie kwenye machafuko kama yaliyotokea mwaka 2000, wakati watu zaidi ya 20 waliuawa na wengine kukimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya ambako waliishi kama wakimbizi.
Lowassa Azungumza
Kwa upande wake, Lowassa aliwataka viongozi wa ngazi za juu wachukue hatua kumaliza mgogoro wa Zanzibar.
“Hili tulichukulie kwa umakini sana. Viongozi wafanye vikao vya maridhiano, tunaipenda sana amani tuliyonayo,” alisema.
Lowassa alisema anashangazwa na jinsi CCM wanavyoshindwa kuheshimu makubaliano ya SUK na kukataa kukubali matokeo.
ZEC yagoma kuondoa picha ya Maalim
Wakati huohuo, habari zinaarifu kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar( ZEC) imegoma kuondoa picha za wagombea Urais,Udiwani na Uwakilishi kutoka vyama vilivyotangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio,ikiwemo jina na picha Maalim Seif Sharif Hamad.
Hilo lilifahamika jana mjini Unguja baada ya kigogo mmoja wa ZEC ambaye hakuwa tayari kutaja jina kusema kuwa sheria hazimruhusu mgombea yeyote kujitoa mwenyewe kwa utashi wake binafsi.
Kiongozi huyo alisema kwa mujibu wa kifungu cha 36 cha sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984,mgombea hawezi kujiondoa kwa utashi wake baada ya Tume kukamilisha kazi ya uteuzi ambayo ilifanyika kabla ya Oktoba 25 mwaka jana.
"Ieleweke kwamba mgombea urais anaweza kujiondoa katika kinyang'anyiro kwa kuwasilisha taarifa za maandishi yeye mwenyewe ofisi za ZEC kabla ya saa 10 jioni ya siku ya uteuzi." Alisema ofisa huyo akinukuu kifungu cha katiba.
Alisema uteuzi wa mgombea mwingine unaweza kufanyika ndani ya siku 21 kama mgombea hatafariki dunia,lakini hakuna ruhusa ya kujitoa kabla ya kukamilika kwa uchaguzi.
Alisema ZEC tayari imeviandikia vyama kuvitaka vithibitishe iwapo wagombea wao wangali hai au kuna waliofariki dunia, na si kutaka kufahamu kama watashiriki uchaguzi wa marudio au la.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi CUF anena
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe amesema ZEC inasuka mkakati wa siri wa kutaka kuzitumia picha na taarifa za wagombea wao kwa lengo la kuidanganya dunia na jumuiya za kimataifa kwamba CUF walishiriki uchaguzi huo.
Shehe amesema CUF kilitangaza mapema kabisa kutoshiriki uchaguzi wa marudio,hivyo dunia nzima inaelewa kabisa kwamba CUF haishiriki uchaguzi huo na kitendo cha kuendelea kuchapisha picha na taarifa za wagombea wao katika karatasi za wapiga kura si sahihi.
Post a Comment