Tamko lililotolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wachimbaji wadogo watapewa mabaki ya mawe ya dhahabu maarufu magwangala kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) limesababisha wakazi wa Mtaa wa Nyakabale kufurika mgodini hapo kusubiri ahadi hiyo.
Vijana hao zaidi ya 800 walisema kuwa wamekusanyika kwa kuwa Serikali ilitangaza kutoa magwangala Februari 28.
Akizungumza na umati wa vijana hao Kaimu Ofisa Madini wa Mkoa wa Geita, Fabian Mshai aliwataka vijana hao kuwa watulivu na kutii sheria za nchi kipindi hiki ambacho tume iliyoundwa kufuatilia suala la magwangala, imepeleka maoni kwa katibu mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kujua utaratibu utakaotumika.
Mshai alisema lazima taratibu zifuatwe ili kuepuka kuhatarisha uhai wa wananchi kwa kugombana wakati wakinyang’anyana mawe.
Alisema pia wanaweza kuharibu mazingira kwa kuwa kuna kemikali kali zinazotumika wakati wa uchanjuaji wa dhahabu.
Alisema kitendo kinachofanywa na wachimbaji wadogo walioamua kuanza kuingia katika maeneo ya mgodi na kuchukua mawe ni kukiuka sheria za madini na kuhatarisha maisha yao.
Diwani wa Mgusu, Pastory Ruhusa aliwataka wachimbaji wadogo kuwa watulivu na kuiomba Serikali kuharakisha taratibu za kutoa magwangala kwa kuwa kuna ongezeko kubwa la wananchi kutokana na ahadi waliyopewa.
Alisema, juzi vijana hao walifunga barabara baada ya kuitwa wakimbizi na kusababisha wananchi kushindwa kusafiri kwenda nje ya kijiji na kusababisha usumbufu kwa wagonjwa na wananchi.
Post a Comment