0
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete amesema hajahusika kufutwa kwa uchaguzi Zanzibar kwa kumpigia simu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Chama ya Kibaha Mjini mkoani Pwani na kusema maneno hayo ni ya uongo, hayana ukweli wowote na watu hawapaswi kutoa shutuma hizo juu yake.

Rais huyo wa Awamu ya Nne alisema maneno hayo hayana kichwa wala miguu wala hajawahi kumpigia simu Jecha kwa ajili ya kuzungumzia masuala ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kwani tume hiyo inajitegemea.

“Wasitoe lawama zisizohusika, wapuuzeni sikuwahi kufanya hivyo hata kwa Damian Lubuva wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania hivyo nashangaa watu wanavyosema kuwa nimehusika kufutwa uchaguzi huo,” alisema Kikwete.

“Tume ya Zanzibar ni tume huru na inajitegemea kwani ina mambo yake hata Dk Ali Mohamed Shein (Rais wa Zanzibar) hana uwezo wa kuingilia na kuahirisha uchaguzi huo, watu hao wasipake watu matope wasio husika kwani kila mtu ana nafasi yake,” alifafanua Kikwete.

Alisema kikubwa kinachotakiwa ni kuwaombea Wazanzibari wafanye uchaguzi wao mkuu wa marudio kwa amani na utulivu ili wapate viongozi wao wa kuiongoza Zanzibar na wawaombee wagombea wa CCM washinde.

Aidha, alisema chama hicho kinapaswa kuwaadhibu watu waliokihujumu chama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kwa kutomwonea mwanachama, bali watende haki na si kwa kwa uonevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao alisema Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka ameonesha njia ya kiongozi kutumia fursa kuboresha mazingira ya utendaji kazi Awali, Koka ambaye ndiye aliyejenga ofisi hiyo yenye thamani ya Sh milioni 100, alisema aliamua kujitolea kujenga ofisi hiyo kwa lengo la kukisaidia chama kiendeshe shughuli zake.

Koka alisema aliamua kujenga kama kumbukumbu kwa wanaKibaha ili iwe kielelezo cha uongozi wake kama mbunge wa Jimbo hilo kwa ajili ya kufanya shughuli za chama badala ya kufanyia sehemu zisizo na hadhi yao

Post a Comment

 
Top