Ni wingu jeusi kwao! Mpaka sasa, Rais Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ ameshawatumbua majipu karibu nusu ya vigogo wa taasisi za serikali lakini habari mpya ni kwamba, maafisa wa usalama wa taifa ‘makachero’ wamekuwa wakishinda kwenye taasisi kubwa za serikali na kupekua nyaraka mbalimbali ili kubaini utendaji uliotukuka au mbovu.
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, makachero hao wamekuwa wakiingia kwa kushtukiza kisha kujitambulisha wao ni akina nani na kuomba nyaraka zinazohusu kitu ambacho wamekwenda kukichunguza.
Omar Bakar – SIDO
MSIKIE MTOA HABARI
“Kinachofanyika sasa ni kwamba, usalama wa taifa wanakwenda kwenye taasisi waliyoilenga, wanaomba nyaraka kutoka kwa wahusika, wanafuatilia utendaji wa taasisi hiyo kisha wanaondoka na majibu mkononi.”
HABARI KWA MAWAZIRI, WAZIRI MKUU
“Kama taasisi ikikutwa na madudu, habari zinapelekwa kwa waziri mwenye dhamana na taasisi hiyo au moja kwa moja kwa Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa.”
Nehemia Mchechu – NHC
ZILITEM-BELEWA
“Taasisi zote ambazo watendaji wake wakuu wametumbuliwa majipu walishatembelewa na watu wa usalama wa taifa. Unajua serikali hii inafanya sana kazi na hawa jamaa. Ndiyo maana kama utafuatilia sana, utabaini kuwa, kila waziri na waziri mkuu akifika mahali penye figisufigisu anasema mambo ambayo kwa akili za kawaida unajua alishaambiwa kabla hajafika.”
Kaimu M James Anditile – TPDC
Chanzo hicho kilizitaja taasisi ambazo zinafuatiliwa na makachero kuwa ni Tanesco (Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania, linaongozwa na Felchesmi Mramba), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC, linaloongozwa na Nehemia Mchechu), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL, inayoongozwa na Kazaura Kamugisha na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC, linaloongozwa na James Anditile).
Kazaura Kamugisha – TCCL
Taasisi nyingine ni Hifadhi ya Taifa Tanzania (Tanapa, inayoongozwa na Allan Kijazi), Shirika la Madini Tanzania (Stamico, linaloongozwa na Edwin Ngonyani) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogovidogo (Sido, linaloongozwa na Omar Bakar).
Pia alizitaja taasisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT inayoongozwa na Ben Ndulu), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura inayoongozwa na Felix Ngamlagosi) na Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra inayoongozwa na Gilliard Gewe).
Edwin Ngonyani – STAMICO
Hata hivyo, chanzo chetu kilisema kuwa, si kwamba kufuatiliwa kwa taasisi hizo ina maana wakurugenzi wake wana madudu.
“Hizi taasisi kama nilivyosema awali, zinafuatiliwa kwa sababu serikali ya Magufuli inataka kujiridhisha katika kila idara. Kama viongozi wake wako sawa watapona na wataendelea na kazi, hakutakuwa na uonevu. Kwa hiyo si kwamba wamebainika kuwa na utendaji mbovu, hapana,” kilisema chanzo hicho.
TANESCO, NHC HAKUKALIKI
Juzi gazeti hili lilipiga hodi Tanesco Makao Makuu jijini Dar kwa lengo la kuzungumza na Afisa Habari, Adrian Sevelin lakini hata hivyo hakuwepo ofisini.
Mfanyakazi mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema hali ya Tanesco kwa sasa ni kazi kwa kwenda mbele kwani bosi wao mkuu, Mramba amekuwa mkali na kufuatilia utendaji wa kazi wa kila mtu.
Ndulu – BoT
“Nyie kama waandishi hapa Tanesco sasa si kama miaka ile. Huyu Mramba, japokuwa hata kabla ya Magufuli alikuwa mkali, lakini da! Sasa hivi mfanyakazi akitoa mguu na yeye kaweka. Anafuatilia utendaji wa kazi wa kila mmoja mpaka pamekuwa pachungu,” alisema mfanyakazi huyo maelezo ambayo yanafanana na ya mfanyakazi mmoja wa NHC.
Gilliard Gewe – Sumatra
Mpaka sasa, taasisi ambazo wakurugenzi au watendaji wake wakuu wameshakumbwa na tumbuatumbua ya Magufuli ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru ambapo mkurugenzi wake, Edward Hosea alitenguliwa uteuzi wake na rais na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA ambapo mtendaji wake mkuu alikuwa Rished Bade).
Felichesmi Mramba – Tanecso
Taasisi nyingine ni Hospitali ya Taifa Muhimbili (mkurugenzi alikuwa Dk. Hussein Kidanto), Kampuni ya Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco, mkurugenzi wake alikuwa Mhandisi Benhadard Tito), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA, mkurugenzi wake alikuwa Awadhi Massawe), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA, mkurugenzi wake alikuwa Charles Chacha).
Nyingine ni Idara ya Uhamiaji Tanzania (mkurugenzi wake alikuwa Sylvester Ambokile), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida, mkurugenzi wake alikuwa Dickson Maimu) na wengine wengi, wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri za wilaya.
Post a Comment