Kasi ya Rais John Magufuli ya kutumbua majipu sasa imeanza kuvunja mtandao wa dawa za kulevya (unga) nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Rais Magufuli ametoa maelekezo mahsusi kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga akielekeza kuwa anataka kuiona Tanzania isiyokuwa na wauzaji na watumiaji ‘unga’.
Rais amenukuliwa akisema haiwezekani wauza unga wakawa na nguvu kuliko Serikali.
Tayari maofisi wa Serikali wameanza kulifanyia kazi agizo hilo kimyakimya na kwa kasi ya aina yake, ambako sasa wanakwenda nyumba hadi nyumba wakihoji wafanyabiashara wenye ukwasi usioelezeka na katika kufanya hivyo wamekutana na ‘maajabu’.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi imeanzisha operesheni ya kukamata wafanyabiashara wote wanaohusishwa na dawa za kulevya jijini Dar es Salaam.
Katika operesheni hiyo, tayari polisi wamekamata ‘mapapa’ wawili wanaoelezwa kuwa miongoni mwa ‘mapapa’ wa biashara hiyo haramu nchini. Mapapa hao wanashikiliwa Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni.
Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni umeanza msako mkali wa kimyakimya kwa wafanyabiashara hao; operesheni inayoelezwa kuwa inahusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idara ya Usalama wa Taifa na kitengo maalum kutoka Ikulu.
JAMHURI limethibitishiwa kuwa Hemed Horohoro na Lwitiko Samson Adam, ni kati ya mapapa waliokuwa wakisakwa kwa udi na uvumba na sasa wametiwa nguvuni.
Lwikito ambaye anaelezwa kuwa na makazi nchini Afrika Kusini, alikamatwa nyumbani kwake Magomeni jijini Dar es Salaam. ‘Papa’ huyo, amekutwa kwenye ‘nyumba ya ajabu’.
“Huwezi kuamini. Lwitiko aliishi maisha ya peponi. Ukiiona nyumba yake pale Magomeni, nje si nyumba ya maana, lakini ukiingia ndani utashangaa. Nyumba imejengwa chini ya ardhi (underground). Huko kuna maisha ya peponi.
“Kule chini ya ardhi ana bwawa kubwa la kuogelea huko huko, baa na magari yote ya kifahari yapatayo manane tuliyakuta huko chini ya ardhi, tulistaajabu,” anasema mmoja wa watu waliofanya kazi ya kumkamata.
Magari yaliyokuwa huko chini ya ardhi mengine yana thamani ya hadi Sh milioni 500. JAMHURI limefanikiwa kupiga picha sehemu ya magari hayo katika Kituo cha Polisi Oysterbay, ambayo yamo BMW X6, Lexus, Lumma CLR RS, Cooper na mengine ya kifahari.
Wakati Lwitiko akikamatwa na baadhi ya mali zake, Hemed alikamatwa na gari moja ambalo nalo pia linashikiliwa katika kituo hicho.
Watuhumiwa hao waliokamatwa wanatajwa kuwa wamekuwa wanauza dawa aina ya heroine kutoka Pakistan; cocaine kutoka Brazil, huku wakiishi maisha ya kifahari nchini Tanzania na Afrika Kusini.
Katika kinachohofiwa kuwa taarifa zimevuja ukamataji ulipoanza wiki iliyopita, kundi kubwa la wafanyabiashara waliolengwa lilikimbia nchi.
“Wengi wamekwenda Kenya na Afrika Kusini. Weengine wameikimbia Dar es Salaam, taarifa za kiintelijensia zinaonyesha wako mikoani, lakini kwa vyovyote vile chini ya Rais [John] Magufuli wanapoteza muda. Watakamatwa tu,” amesema mtoa habari wetu.
Kamanda wa Polisi Kanda ya Kinondoni, ACP Christopher Fuime, anasema ukamataji huo ni endelevu, lakini hakutaka kuingia kwa undani zaidi akisema wananchi wasubiri kuona ‘wazungu wa unga’ wote wanapotea mtaani.
Anasema kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya si watu wadogo, bali wana uwezo na wanamiliki mtandao mkubwa, hivyo kukabiliana nao kunahitaji “muda na usiri mkubwa”.
Alipoulizwa ni lini wanatarajia kuwafikisha mahakamani ‘mapapa wawili’ waliokamatwa, amesema hawezi kuzungumzia hilo kwani upelelezi bado unaendelea na kwamba unahusisha taasisi nyingi, hivyo ni vigumu kubainisha hilo.
Hata hivyo, amekiri kukamatwa kwa Horohoro na Lwitiko na anasema: “Hapa tunafuatilia mambo mengi. Tunavyopeleleza kesi za dawa za kulevya tunaangalia umiliki wa mali, utakatishaji wa fedha, na mambo mengine mengi. Ila kwa sasa tumeamua ingawa wengine wanakimbia baada ya kubonyezwa, lakini hiyo siyo tatizo,” anasema Kamanda Fuime.
Katika eneo la kutakatisha fedha za dawa za kulevya, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanamiliki mabasi yanayofanya kazi ya daladala jijini Dar es Salaam na mengine yanakwenda mikoani.
“Mabasi haya mengi yanatoka Mbagala kwenda Posta, yameandikwa jina la moja ya taasisi kubwa za uzalishaji mafuta duniani, na pembeni yameandikwa majina yao kwa kuongeza herufi mbili mwishoni tu zisomekazo ‘so’. Huyu anaingiza hadi kilo 500 ze heroine kutoka Pakistan, na fedha anazopata anazitakatisha kwa kuonyesha anafanya biashara ya daladala na mabasi ya mikoani,” amesema mtoa habari wetu.
“Wiki iliyopita, Wapakistani sita wameingiza kilo 500 za heroine, wakahifadhi robo Segerea jijini Dar es Salaam, nyingine zimehifadhiwa Pemba, nyingine Zanzibar na nyingine zipo kwenye boti majini hazijaingia nchini,” kiliongeza chanzo chetu.
Ukiacha magari, wanaouza dawa za kulevya wanajenga majengo makubwa katika miji ya Dar es salaam, Zanzibar, Arusha, Mwanza, Tanga na Mbeya, kisha wanatumia majengo hayo kudanganya umma kuwa fedha zao zinatokana na kodi ya pango.
Kamanda Fuime, alipoulizwa mkakati wa kupambana na wauzaji waliotajwa kuikimbia nchi, amesema kuzungumzia hilo ni sawa na kuanika mipango ya polisi; jambo ambalo si sahihi.
Miezi miwili iliyopita polisi nchini walifanya uhamisho kwa askari wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni na Tanga kuvunja mtandao wa uhalifu, hususan dawa za kulevya ndani ya Jeshi hilo.
Asilimia kubwa ya ‘mapapa’ wa biashara hiyo haramu wapo jijini Dar es Salaam, hasa maeneo ya Kinondoni, Magomeni na Mbezi Beach.
Waziri Kitwanga ameshakabidhiwa orodha ya polisi wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ambako majina hayo aliyakabidhi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Inspekta Jenerali Ernest Mangu.
Baada ya IGP Mangu kukabidhiwa majina hayo, aliwataka askari wa Oysterbay kumkabidhi orodha ya majina ya wauza ‘unga’ haraka.
Mpango huo ulienda sambamba na kuwapangua baadhi ya polisi walioonekana kushindwa kuukabili mtandao wa wauza ‘unga’.
Maofisa waliohamishwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Kinondoni Camillius Wambura, aliyepelekwa Manyara na Mkuu wa Utawala Kinondoni, pamoja na baadhi ya askari wa kitengo cha upelelezi na wengine kutoka idara mbalimbali.
Kuhamishwa kwao kulitokana na kushindwa kwao kudhibiti mtandao wa dawa za kulevya nchini, kiasi cha kuifanya Tanzania kuwekwa kwenye orodha ya nchi zinazojihusisha na biashara hiyo kwa kiwango cha juu.
Awali, kabla ya matukio hayo, Tanzania ilikuwa ikitumiwa kama njia ya kupitishia dawa za kulevya kwenda Afrika Kusini, Ulaya na Amerika, lakini kadri siku zinavyokwenda inakuwa soko la dawa hizo.
Kinachotokea vijana wengi mitaani wanaoitwa mateja, ndiyo wenye kufanya kazi ya kuiba na kupora vitu vya watu mbalimbali. Fedha wanazopata wanazitumia kununua ‘kete za dawa’ na kuzitumia.
Kundi hili limeongezeka, na inaelezwa kuwa wafanyabiashara vijana wa kundi la kati wengi sasa wanatumia dawa za kulevya na hilo ndilo linachangia magari mengi kuwekewa ‘tinted’, kwa nia ya kuficha maovu.
Serikali ya Awamu ya Nne, iliamua kupambana na dawa za kulevya kwa kubadili sheria na ikaelekeza kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, lakini hadi leo chombo hicho hakijaundwa.
Ukiacha kutoundwa kwa chombo hicho, wafadhili walikuwa wakitoa fedha za kununulia dawa ya methodine kwa ajili ya vijana walioathirika na dawa za kulevya, lakini maofisa waliopo katika Tume ya Dawa za Kulevya wakaishia kuzifuja na hivyo mradi ukafutwa.
Matumaini makubwa ya Watanzania sasa yapo mikononi mwa Rais Magufuli, kwani inaelezwa kuwa yeye hana ushirika na wafanyabiashara ambao baadhi yao wanafanya biashara ya dawa za kulevya.
“Tunachosema, Rais sasa achunguze wanaomiliki mabasi, majumba makubwa na biashara zisizoelezeka mitaji yake ilipatikanaje, kisha kuanzia hapo atajua kina nani wanafanya biashara haramu na kina nani wanatumia biashara kutakatisha fedha za dawa za kulevya,” ameshauri mtoa habari wetu.
Gazeti la JAMHURI limekuwa miongoni mwa vyombo vya habari vilivyo mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Mwezi uliopita lilichapisha orodha ya wauza unga 560 wanaofanya biashara hiyo nchini, na ambao wengi wao wapo mikononi mwa dola kwa sasa.
Hata hivyo, kumekuwapo madai kuwa wanaokamatwa wengi ni wachuuzi wa chini na wa kati, lakini wahusika wakuu wanaogharimia biashara hiyo, wakiwamo viongozi serikalini na katika vyombo vya dola, wakiwa hawajakamatwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment