Mungu ni mwema hatuna budi kumshukuru kwa anayotufanyia katika nchi yetu.
Baada ya kusema hayo niseme bila kumung’unya maneno kwamba Rais Dk. John Pombe Magufuli ndiye rais tuliyekuwa tunamtaka kutokana na anachokifanya sasa.
Nichukue nafasi hii kumpongeza kwa hatua anazochukua ili kuwafanya wananchi wanufaike na rasilimali za nchi hii, hivyo namtakia kila la heri katika kazi yake ya kututumikia. Naomba kukiri kwa uwazi kwamba Watanzania tulifanya chaguo sahihi, hatukukosea.
Tanzania ina vyama 23 vya siasa vilivyosajiliwa na vinavyofanya kazi sasa, tutake tusitake Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilimuona Dk. Magufuli kuwa ni tunu ya taifa na leo anadhihirisha hilo kwa kupigania wananchi wake na kuwa adui kwa mafisadi.
Kila Mtanzania sasa anaamini kwamba Dk.Magufuli anaweza kurejesha bila wasiwasi usimamizi thabiti wa serikali na nidhamu ya utendaji ndani ya serikali. Naamini kuwa serikali ya Magufuli itakuwa ya kiusimamizi na yeye mwenyewe anaweza kulifanya jambo hilo bila kusita. Tumeona.
Katika nyadhifa nyingi alizopitia hadi sasa ameijenga taswira hii kila alikopita na bado inambeba katika awamu hii ya tano.Hakuna siri, kama kuna jambo ambalo lilikuwa haliendi sawa nchini ni la utendaji ndani ya serikali. Tunafahamu kuwa wafanyakazi ndani ya serikali ukiachilia mbali matatizo waliyonayo kwa maana ya vipato, hata mambo madogo ambayo wangeweza kuyasimamia ndani ya dakika au saa chache yalichukua wiki hata miezi kadhaa.
Utaratibu wa utoaji huduma ulikwama sana lakini kwa spidi ya Rais Magufuli atafanikiwa kutatua changamoto hiyo kubwa na ya siku nyingi. Ikiwa utendaji wa serikali unaimarika na huduma zinatolewa kwa wakati, tutaweza kujenga taifa linalokwenda mbele kimaendeleo.
Taswira bora ya pili ya serikali ya Dk. Magufuli ni misimamo katika masuala ya msingi na kutoyumba. Magufuli muda wote ambao amekuwa kiongozi anaonesha njia, ndiyo maana alipoanza tu kazi, alianza na tabia ya ziara za kushtukiza. Hii alikuwa akifanya hata alipokuwa waziri wa ujenzi.
Moja ya mambo ambayo serikali iliyopita ilikosa ni pamoja na kukosa misimamo na kuwa na Double standard. Mfano mdogo tu ni kwenye mchakato wa Katiba Mpya ambapo rais anayeondoka alisimamia uanzishwaji bora wa mchakato huo, akaunga mkono katika hatua zote na rasimu zote, lakini akaja kuwageuka wajumbe wa tume hiyo na rasimu yao ya pili alipolihutubia Bunge Maalumu la Katiba.
Naamini Magufuli si mtu wa kugeuka na kuna masuala mengi anaweza kuyasimamia kwa dhati na kila mmoja wetu akakubali kuwa, huyu ni kiongozi anayesimamia haki na ana uchungu na wananchi wake.
Amekuwa akitetea wanyonge hadharani mara nyingi na anaonekana wazi kwamba anaumizwa na watu wanaoibia serikali bila kujali kuwa kuna watu wanakosa mlo mmoja kwa siku.
Wote tumuunge mkono, ni rais anayestahili sifa hizo, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Kwa kufanya hivyo naamini tutashinda.
Jipu limepasuka siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Post a Comment