Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, amesema hatazungumzia lolote kuhusu utendaji wa Rais John Magufuli katika siku 100 za kwanza tangu aingie Ikulu.
Awali, mwanasiasa huyo ambaye mwishoni mwa mwaka jana alikihama chama alichokiasisi na kukitumikia kwa zaidi ya miaka 60, aliliahidi gazeti hili kuwa atazungumzia utendaji wa Rais atakapofikisha siku 100 madarakani.
Kingunge alisema mapema mwaka huu kuwa marais na viongozi mbalimbali hupimwa ndani ya siku 100, hivyo alitaka apewe muda hadi siku hizo zitakapotimia.
Lakini Kingunge alipotakiwa kutoa maoni yake jana mara baada ya Rais Magufuli kutimiza siku 100 tangu aingie Ikulu Novemba 5 mwaka jana, alikataa katakata kusema lolote na kumweleza mwandishi wa gazeti hili kuwa hakuna wa kumlazimisha kuzungumza.
“Hata kama niliahidi kuzungumza baada ya siku 100 kama unavyosema lakini hakuna mwenye uwezo wa kunilazimisha kuzungumza,” alisema Kingunge. "Sitazungumza, waulizeni wengine watasema ila mimi naomba mniache."
Kingunge ambaye alikuwa na kadi namba 8 ya CCM kabla ya kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumpigia kampeni aliyekuwa mgombea urais wa Chadema kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Edward Lowassa, alisema ni mapema mno kumjadili Magufuli.
Wakati Kingunge akiahidi kuzungumza baada ya siku 100, Rais Magufuli alikuwa ametimiza siku ya 59 tangu aingie madarakani mwaka jana.
“Jamani ni mapema mno kumpima, msiwe na haraka nitatoa maoni yangu wakati huo ukifika kwasasa mwacheni afanye kazi zake msimwingilie ingilie,” alisema Kingunge ambaye aliwahi kushika nyadhifa nzito serikalini na kwenye CCM.
Kingunge alisisitiza kuwa hakuna haraka ya kuanza kumchokonoa Rais na badala yake aachwe atekeleze majukumu yake na tathmini atafanyiwa baada ya siku 100 akiwa Ikulu.
Oktoba 4 mwaka jana, Kingunge alitangaza rasmi kujiengua CCM, akisema alifanya hivyo kutokana na kile alichokiamini kuwa CCM haifanyi yaliyoasisiwa na kujengewa misingi bora na waasisi wake.
Wakati akitangaza uamuzi huo, alisema hakusudii kuhamia chama chochote cha siasa nchini bali atakuwa mtanzania huru lakini muda si mrefu aliungana na Ukawa kumnadi Lowassa.
Mwanasiasa huyo ambaye sehemu kubwa ya maisha yake alikuwa CCM, alisema wananchi wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya chama hicho, ikiwa ni nukuu ya nasaha maarufu iliyowahi kutolewa na Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment