0
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Jakaya Kikwete amesema kuwa chama chake kitawachambua na kuwaadhibu wote ambao walikisaliti katika Uchaguzi Mkuu uliopita, kuanzia ngazi za matawi, kata, wilaya, mkoa hadi Taifa.

Dk. Kikwete ametoa kauli hiyo Jumatatu ya wiki hii mjini Kibaha alipohudhuria sherehe za uzinduzi wa ofisi mpya ya chama hicho mjini humo.

“Baada ya mchakato wa Dodoma wapo ambao walisusa kabisa na wakawa wanajificha. Unakuta hahudhurii mikutano yetu ya kampeni, lakini ya wenzetu upinzani unamkuta na akiulizwa anasema eti alialikwa,” alisema na kusisitiza kuwa wanachama kama hao ni wasaliti na uanachama wao una mashaka.

Kikwete alisema mchakato wa kuwaadhibu wanachama wasaliti utafanyika wakati wowote baada ya kuyapitia majina ya wote wanaotuhumiwa kukihujumu chama.

“Tayari tuna majina ya watu ambayo yanadhaniwa walikihujumu chama. Tutayapembua katika vikao mbalimbali halali kuanzia ngazi za matawi, kata, wilaya, mkoa na Taifa na tutaamua kwa haki wakati wa kuwaadhibu,” alisema.

Aliwataka wanachama hao kufanya tathmini na kutambua waliokisaliti chama lakini alionya vikao vya kuwabaini vitende haki bila kumuonea mtu akisema yapo baadhi ya majina yanatajwa kuwa ni wasaliti kutokana na migogoro binafsi baina yao.

Post a Comment

 
Top