Chama cha Wananchi (CUF) kimesema ikitokea Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad ameshinda kwa kupigiwa kura na akaibuka mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi wa marudio utakaofanyika Machi 20, hatakwenda kuapishwa.
Kimesema kuna uwezekano mkubwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ikaweka jina la Maalim, wawakilishi na madiwani katika karatasi za kupigia kura na kusisitiza, ikitokea hivyo na wagombea hao wakapigiwa kura, wote hawataenda kuapa.
“Kama wagombea wetu wakichaguliwa na ZEC ikawatangaza washindi itakuwa ni kazi bure. Pia, CUF hatutakwenda mahakamani kufungua kesi ya kikatiba kupinga hatua ya mwenyekiti wa ZEC kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25,” Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui aliwaambia waandishi wa habari jana.
Oktoba 28, mwaka jana mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi wa rais, wawakili shi na madiwani kwa maelezo kuwa sheria na kanuni zilikiukwa na baadaye kutangaza Machi 20 kuwa siku ya kupiga kura upya.
Mazrui alisema licha ya CUF kuiandikia barua ZEC, ikitaka wagombea wake wote kuondolewa katika orodha ya karatasi ya kupigia kura, kuna uwezekano mkubwa wa majina hayo kutoondolewa.
“... Sisi tumeshaipelekea ZEC barua 54 za wawakilishi na madiwani walioshindwa au kushinda katika uchaguzi wa Oktoba 25 na kuwaeleza kuwa wawaondoe katika karatasi za uchaguzi wa marudio.
"Hata kama wananchi watamchagua Maalim Seif kwa asilimia 90 hawezi kwenda kuapishwa. Kufanya hivyo ni sawa na kukataa kula nyama ya nguruwe lakini mchuzi wa nyama hiyo unaunywa.”
Mazrui ambaye alitangazwa mshindi wa uwakilishi wa jimbo la Mtopepo, kabla ya kufutwa kwa matokeo hayo alisema, “Hatuna shida na uchaguzi wao, tumekosa nini mpaka tuwe na shida nao?”
Alisema CCM inadhani kwamba CUF itajitosa kushiriki uchaguzi huo wa marudio katika dakika za mwisho; “wanachotakiwa kujua ni kwamba hatuingii katika uchaguzi wao wawe na amani yote.”
Akizungumzia kauli ya Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu kwamba CUF walipaswa kupinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi, siku 14 baada ya kutangazwa, Mazrui alisema kauli hiyo imedhihirisha kuwa hata wakienda mahakamani hakuna haki itakayotendeka.
“Ameshatoa hukumu kabla hata kesi haijafunguliwa. Muda wa siku 14 aliousema unahusu ukomo wa kupeleka kesi ya uchaguzi Mahakama Kuu. Kesi ya uchaguzi msingi wake mkubwa ni uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi ambao CUF na wajumbe wateule hatuna tatizo nao,” alisema.
“Hakuna anayetaka atangazwe mshindi kati ya wagombea wote wa CUF kwa kuwa walitangazwa kihalali na wasimamizi wa uchaguzi na kupewa vyeti.
"Aliyehujumu uchaguzi si ZEC ni Jecha. Sisi kesi tunayoweza kufungua ni ya kikatiba si kupinga matokeo na kesi ya kikatiba haina muda wa kufungua kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.”
Alisema kutokana na kauli ya Makungu, CUF imewashauri wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliokuwa na nia ya kupeleka shauri mahakamani kuachana na wazo hilo kwa maelezo kuwa Jaji Makungu ameshaandaa hukumu na kuisoma hadharani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment